Published On: Tue, Jul 31st, 2018

Serikali kumnyang’anya mashamba Mohammed Enterprises.

Share This
Tags

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Angelina Mabula amesema serikali imekusudia kuchukua baadhi ya mashamba yanayomilikiwa na Kampuni ya Mohammed Enterprises na kuwapa wananchi kwa kuwa wameshindwa kutimiza masharti ya uendelezaji wake.

Mabulla amesema hayo baada ya kufanya ziara ya ukaguzi wa mashamba katika Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga ambapo amegundua kampuni ya Mohammed Enterprises inamiliki maeneo makubwa sana kwa zaidi ya hekta 9,418 sawa na hekari 20,779 ambayo wamechukulia mkopo kwa ajili ya kupanda mkonge, kitu ambacho hakijafanyika kwa asilimia kubwa.

Naibu Waziri Mabulla amefanya ziara ya ukaguzi wa mashamba yote 14 yanayomilikiwa na Kampuni ya Mohammed Enterprises na kugundua kuwa amepanda mkonge eneo dogo sana na sehemu kubwa ni mapori tofauti na taarifa aliyopewa na kampuni hiyo.

Pia amesema mashamba hayo yametumika kuchukua mikopo benki lakini mikopo hiyo haijatumika kuendeleza mashamba hayo kitu ambacho kinafanya wananchi wayahitaji maeneo hayo lakini wanashindwa kuyatumia kwa kuwa yanamilikiwa na kampuni hiyo.

Akijatetea mbele ya Naibu Waziri wa Ardhi Meneja anayesimamia Mashamba yote ya mkonge ya kampuni ya Mohammed Enterprises Newalo Nyari, amesema si kweli kwamba hawajaendeleza maeneo hayo bali wameendeleza na wamepanda mkonge baadhi ya maeneo na mengine wameyaacha mapori ili kuhifadhi misitu na mengine wanawaachia wananchi waweze kupanda mazao yao ikiwa ni ushirikiano wa kijirani.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Handeni aliyekuwa akikaimu nafasi ya Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Godwin Gondwe, ambaye ameonesha kukasirishwa na maneno ya meneja huyo kwamba wameendeleza mashamba hayo wakati yeye mwenyewe ameshuhudia kwa macho yake mashamba yote 14 na kuona hali halisi ya mapori ambayo hayajaendelezwa.

Baadhi ya wananchi wa Korogwe wameonesha kufurahishwa na hatua hiyo ya Serikali ya kuipunguzia umiliki wa baadhi ya maeneo yanayomilikiwa na kampuni ya Mohammed Enterprises ambayo watapewa wananchi hao ili waweze kufanya shughuli zao za maendeleo.

Posted By

-

Leave a comment

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>