Published On: Tue, Jun 12th, 2018

MALIMA ANAYEISHI KWA MSHAHARA WA ELFU 90 TU KWA MWEZI

Share This
Tags

“Kwa jina ninaitwa Malima Abel Konzery ninaishi Dodoma, Chigongwe lakini nafanya kazi eneo la Mji mpya hapa Dodoma. Ninafanya kazi kwa watu binafsi kwa makubaliano tu sio kama  nina mkataba maalum kamvile watu wa serikalini” Hivi ndivyo anaanza kuzungumza kwa unyonge Malima mwenye umri 29 tu ambaye pamoja na kufanya kazi kwenye mazingira magumu lakini anapata kipato kudogo chini ya kima cha chini.

Malima anaeleza kuwa analipwa shilingi 90,000 pekee kwa mwezi kwa kazi ya kufanya usafi na kufua katika nyumba ya kulala wageni iliyopo eneo la mji mpya mjini Dodoma. Malima anaeleza kuwa pamoja na kipato hicho lakini huwa anapata kifungua kinywa hapohapo kazini kila siku na ili kubana matumizi yeye hupata mlo mmoja pekee kwa siku unaogharimu shilingi 1,000 hivyo kwa mwezi mmoja hutumia takribani shilingi 30,000 kwa ajili ya chakula sawa na zaidi ya asilimia 30 ya kipato chake. Anaeleza zaidi kuwa matumizi yake kwa mwezi kwa ujumla yanafikia shilingi 60,000 huku akijiwekea akiba ya shilingi 30,000.

Kwa mujibu wa hesabu kutoka https://haliyangu.habariclouds.com mshahara wa kima cha chini Tanzania ni Sh 33,4500 kwa mwezi hivyo Malima amekuwa akilipwa asilimia 26 pekee ya mshahara wa kima cha chini sawa na Sh 90,000 kwa mwezi kiasi kinachomuwezesha kukidhi asilimia 19 pekee ya mahitaji yake ya msingi.

Malima ambaye alihamia Dodoma akitokea jijini Dar es Salaam alipokuwa akifanya kazi ya uchuuzi wa bidhaa almaarufu kama machinga baada ya kile anachoeleza gharama za maisha kumshinda  anasema kuwa kwa sasa halipi kodi ya chumba cha kuishi kwani yeye hana chumba cha kuishi bali huwa anapumzika mchana tu katika kibarua chake cha kwanza baada ya kumaliza kazi za usafi kabla ya kuelekea kwenye kibarua chake cha pili cha ulinzi usiku.

“Sina chumba hapa mjini nikitoka hapa naenda kulinda sehemu nyingine usiku, nikimaliza kazi zangu za mchana hapa nalala kidogo kisha jioni naingia kazini tena”. Anafafanua Malima. 

Pamoja na udogo wa kipato chake Malima ambaye hana mke wala mtoto anaeleza kuwa kila mwezi hutenga angalau shilingi 20,000 sawa na takribani asilimia 22 ya kipato chake kwa ajili ya wazazi wake ambao pia wanaishi Dodoma. Anasema endapo angebahatika kupata elimu basi angependa sana kujiunga na jeshi kwani ni kazi aliyokuwa akiipend kuanzia akiwa mtoto mdogo.  

Malima hajivunii, hapendi na anakerwa na kazi aifanyayo sasa kwani anaeleza kuwa anafanya kazi kubwa lakini kipato anachopata ni kidogo  kulinganisha na kazi afanyayo.

“Kipato kipo chini sana, kazi ninayofanya ni kubwa lakini kipato kipo chini kwa hiyo hata nikiwa na familia siwezi kushauri afanye kazi kama yangu” Anaeleza Malima akionyesha kuwa hawezi kumshauri mwanaye kufanya kazi kama aifanyayo yeye kwani yeye mwenyewe haridhiki nayo.

Kutokana na hali ngumu ya maisha Malima anaeleza kuwa kama akiwa na mahitaji ya muda wa mawasiliano kwenye simu kiwango cha juu anachoweza kumudu kuweka ni shilingi 1,000 lakini mara nyingi anasubiri apigiwe simu, na kama akipenda nguo kiwango cha juu anachoweza kumudu ni shilingi 20,000 tu na haiwezi kuzidi hapo

 

Posted By

-

Leave a comment

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>