Published On: Wed, Jun 20th, 2018

Hali Yangu: Maisha ya Siwema na Changamoto za Mshahara wa 80,000 kwa Mwezi

Share This
Tags

Siwema Juma (25), ni mkazi wa Buguruni Kwa-Mnyamani, jijini Dar es Salaam anafanya kazi kwenye mazingira magumu kama mhudumu wa baa (almaarufu baamedi) jijini Dares Salaam.

Anaonekana ni mwenye tabasamu, mrembo na mwenye kujipenda lakini kutokana na kipato kidogo apatacho katika kazi yake hawezi kumudu kukidhi mahitaji yake muhimu kama binti wa kisasa, yakiwamo mavazi yenye kuvutia pamoja na kulipia nyumba nzuri ya kuishi.

Ili kupunguza ukali wa gharama za maisha, Siwema pamoja na rafiki zake wawili wanaishi katika chumba kimoja kinachogharimu shilingi 15,000 kwa mwezi, hivyo kila mmoja huchangia kiasi cha shilingi 5,000.
Chumba hicho hakina sakafu nzuri, ni kidogo sana na hakuna huduma muhimu kama maji huku umeme ukipatikana kwa taabu sana kwa njia ya malipo ya “LUKU”.

Kutokana na changamoto ya kipato pamoja na mafanikio duni aliyoyapata kwa zaidi ya miaka mitano ya kazi ya kuhudumu katika baa, Siwema alijikuta ameingia katika biashara ya ngono ili angalau apate kipato cha ziada kuweza kumudu mahitaji yake ya kila siku.

“Maisha ni magumu sana, pamoja na kuwa nafanya kazi ngumu ya kusimama na kuzunguka zaidi ya masaa 10 kila siku nalipwa mshahara wa shilingi 80,000 tu kwa mwezi ambayo haikidhi mahitaji yangu kabisa. Ninalazimika kukubali ofa za wateja ninaowahudumia, na wakati mwingine kulazimika kulala nao baada ya kazi na hunilipa kuanzia shilingi 5,000 au zaidi, pesa ambayo inanisogeza”. alisema.

Kwa mujibu wa mahesabu kutoka haliyangu.habariclouds.com mshahara wa kima cha chini Tanzania ni Sh 33,4500 kwa mwezi. Siwema amekuwa akilipwa asilimia 24 pekee ya mshahara wa kima cha chini sawa na Sh 80,000 kwa mwezi.

Siwema anaeleza kuwa hutumia shilingi 3,000 kila siku kama gharama ya chakula ikijumuisha pia gharama ya vocha ya shilingi 500, hii inamaanisha kuwa kwa mwezi mmoja gharama ya chakula na “vocha” ni takribani shilingi 90,000.

Gharama zote hizi hazijumuishi gharama za afya, elimu na usafiri. Siwema
anasema kuwa hawezi kuhimili gharama za afya kwa sababu hana bima ya afya na anaeleza kuwa pale anapohisi mwili wake haupo sawa basi yeye humeza Panadol (dawa za kutuliza maumivu). Anaongeza kuwa, kwa kuwa anapoishi ni karibu na sehemu ya kazi hana gharama za usafiri na pia hana mtu anayemtegemea kielimu.

Si Siwema pekee nchini Tanzania anayeishi chini ya kiwango kutokana na kipato kidogo, Titus Zakayo pamoja na mkewe Esther Yohabu na mtoto wao mmoja pia wanaishi chini ya kiwango. Akijishughulisha na kazi ya ulinzi na utunzaji wa bustani Titus analipwa mshahara wa shilingi 150,000 kama mlinzi na mtunza bustani hivyo kumfanya yeye na familia yake kuiishi chini ya kiwango kwa asilimia 49 ya mshahara ambao kulingana na haliyangu.habariclouds.com Titus anapaswa kulipwa 305, 000.

Titus anaishi chini ya kiwango huku sehemu kubwa ya matumizi yake ikiwa kwenye gharama ya chakula. “Kwa mwezi mimi na familia yangu tunatumia si chini ya shilingi 180,000 ambayo haitoshi na hapo pia napata msaada wa baadhi ya vyakula kutoka kijijini katika shamba langu lililopo Dodoma” Anaeleza Titus

Gharama nyingine ambazo ni kubwa ni zile zinazohusu matibabu. Titus anaeleza kuwa “hana uwezo wa kulipia bima ya afya kwa ajili ya familia yake hasa kwa mtoto wao mdogo mwenye umri wa miaka miwili.
“Mara nyingi hujikuta tukimpeleka zahanati au hata kununua tu dawa katika maduka ya dawa bila kujua haswa tatizo ni nini. Gharama za matibabu zipo juu sana kuanzia vipimo hadi tiba hivyo inatubidi
tukiona ana joto tunaenda duka la dawa na kuongea na muuzaji tunapata dawa”. anaongeza Titus mwenye miaka 37.

Titus anafafanua kuwa kazi anayoifanya haimuingizi kipato kikubwa lakini ni afadhali kuliko kukosa kabisa. Anasema kuwa hofu yake kubwa ni pale mtoto akifika umri wa kuanza shule. “Nafikiria jinsi ya kujiongezea kipato, maana mtoto anakua na inabidi nijipange gharama za kumsomesha katika shule nzuri kuanzia mwanzo kwani sipendi mwanangu naye aje awe kibarua”.

Posted By

-

Leave a comment

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>