Published On: Wed, Jun 20th, 2018

Hali Yangu: Changamoto za Kipato Kidogo na Maisha ya Dar es Salaam

Share This
Tags

Samantha Mdee mwenye umri wa miaka 26 ni mtoto wa pekee kwa baba na mama yake. Alihitimu elimu yake ya Sekondari katika shule ya wasichana ya Rose Marie iliyopo Kibaha mkoani Pwani. Kwa sasa Samantha ni mama wa mtoto mmoja na anafanya kazi ya “hotelia” katika moja ya hoteli iliyopo eneo la Posta jijiini Dar es Salaam Samantha anasema kuwa mara baada ya kumaliza elimu yake ya Sekondari alishauriwa na wazazi wake kusomea masomo ya uhasibu kwa sababu hakuwa na wastani wa ufaulu ambao ungemuwezesha kuendelea na masomo ya ngazi za juu. “Ilinibidi kusoma kuanzia ngazi ya cheti na baada ya hapo nikasomea tena mambo ya “air fare tickets” na mara baada ya kumaliza nilibahatika kupata kazi”. Anasema Samantha

Samantha anaeleza kuwa hakutarajia kufanya kazi aifanyayo sasa, ila alishawishiwa na msukumo wa watu waliokuwa wamemzunguka hasa wazazi wake lakini kwa sasa anaipenda kazi yake kwa sababu inampa mahitaji yake ya kila siku japokuwa haikidhi mahitaji yake yote. “Mimi nilipenda sana kufanya kazi katika ndege kama mhudumu wa ndege (air hostess), hii ndio ilikuwa ndoto yangu tangu nikiwa mdogo, ila kadri muda ulivyozidi kwenda ndivyo mambo yalivyokuwa yakibadilika, wazazi wangu wanataka hiki mimi nataka kile ikawa ni mvutano lakini ilifika kipindi ikabidi mimi kama mtoto nifuate ushauri wa wazazi. Mwanzoni sikuipenda hii kazi kabisa ila nilikuja kuipenda baadaye, unajua watoto wengi huwa hatusemi kile ambacho kipo katika akili zetu sababu ya woga mwisho wa siku tunajikuta tunafanya kazi ambazo hatukutarajia”. Anaongeza Samantha

Samantha anaeleza kuwa ndoto zake za kuwa mhudumu katika ndege zilifika mwisho mara baada ya kujifungua kwani ilibidi awe karibu na mwanaye na pia hakuwa na mtu ambaye angeweza kumsaidia kumtunza mwanae endapo yeye angesafiri hasa ikizingatiwa kazi ya uhudumu katika ndege ingempasa kusafiri mara kwa mara. Anafafanua kuwa majukumu yake ya kila siku kama “hotelia” huanza kwa kuangalia wageni gani wanatakiwa kuondoka hotelini (check out) na wanaopaswa kuingia hotelini (check in) Kwa kazi hiyo yeye hulipwa mshahara kati ya laki nne na laki tano (400,000-500,000) kwa mwezi.

Samatha anasema kuwa kwa kipato anacholipwa kinasaidia kulipa baadhi ya vitu na pia hujiongezea kipato cha ziada kwa kuuza baadhi ya bidhaa kutoka Zanzibar. “Kiukweli bila kuwa na biashara pembeni nisingeweza kuendesha maisha yangu hapa mjini. Ninaishi katika nyumba ya kupanga ambayo ninalipia kodi ya pango shilingi 80,000 kwa mwezi, ninalipa umeme (luku) shilingi 50,000 kwa mwezi, gharama ya chakula ni shilingi 5,000 kila siku pamoja na shilingi 50,000 kwa mwezi ambayo ninamlipa binti anayenisaidia kumtunza mtoto wangu. Mbali na hiyo kuna shilingi 100,000 ambayo huwepo kwa matumizi ya dharura yanayojitokeza pale nyumbani”. Anaongea Samantha

“Wajua mimi ni jasiri na sina aibu, na aina hii ya biashara ninayoifanya mtu hutakiwi kuwa na aibu. Hata ukinitazama jinsi nilivyo unaweza usiamini kama ni mimi nauza ubuyu, udi au sabuni ila nafanya haya yote ili niweze kupata pesa halali ya kujikimu, biashara hizi hunisaidia kupata pesa ya matumizi ya chakula nyumbani kwangu hivyo najikuta situmii kabisa mshahara wangu katika matumizi ya chakula”. Anasema Samantha

Samantha anaendelea kusema hana ugumu sana kimaisha sababu pamoja na kwamba ana mtoto mwenye umri wa miaka mitano na ambaye ameshaanza shule ya awali. Jukumu la ada kwa mtoto wake ambayo ni shilingi 800,000 kwa mwaka limebebwa na baba wa mtoto mwenyewe na hivyo kumfanya apate unafuu wa maisha. Pamoja na kupata sapoti kutoka kwa mzazi mwenzie Samantha bado anaishi chini ya kiwango cha mshahara wake.

Kwa mujibu wa mtandao wa mahesabu kutoka haliyangu.habariclouds.com Samantha amekuwa akiishi kwa mshahara wa chini ya asilimia 37 kwa mwezi sawa na mshahara kati ya laki nne na laki tano, Kwa mujibu wa mtandao huo Samantha anapaswa kulipwa mshahara wa shilingi 950,136 kila mwezi. Kumbuka asilimia 37 ya mshahara wa Samantha haihusishi gharama za usafiri, mawasiliano na matibabu kwani amekuwa akipata unafuu wa usafiri kutoka ofisini kwake, na ana kadi ya bima ya afya ambayo inatumika kwake yeye na mwanaye na kwa upande wa mawasiliano.

Samantha analipiwa matumizi kwa mwezi na ofisi yake hivyo hana matumizi ya kununua muda wa mawasiliano. “Kiukweli sina gharama kubwa sana katika usafiri na haitoki katika mshahara wangu kwa sababu mara nyingi hurudishwa na gari ya ofisi hasa pale napokuwa natoka usiku na kwa upande wa asubuhi huwa napata lifti kutoka kwa rafiki yangu mmoja. Pia ikitokea kuwa natakiwa kupanda daladala basi hutumia zile pesa ambazo napata kama “tip” kutoka kwa wateja,” anaongeza Samantha

Posted By

-

Leave a comment

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>