Published On: Thu, May 17th, 2018

NYUMBA NA VYOO VYABOMOKA KWA MVUA KILIMANJARO

Share This
Tags

Zaidi ya Nyumba 130 na vyoo 182 vimebomoka mkoani Kilimanjaro kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha huku zaidi ya ekari 4,000 za mazao mbalimbali kama Mahindi Mpunga, Maharagwe na Migomba zikiharibiwa vibaya nyingine zikizingirwa na maji .

Taarifa hiyo ilitolewa katika kikao cha uzinduzi wa kamati ya Maafa ya mkoa wa Kilimanjaro kilichowakutanisha wajumbe kutoka taasisi mbalimbali zikiwemo za kidini, wafanyabiashara, wataalamu mbalimbali pamoja na kamati ya ulinzi na usalama.

Maeneo yanayotajwa kuathirika zaidi na mvua za masika ni pamoja na maeneo ya wilaya za Moshi, Mwanga, Siha, Hai na Same huku kaya zaidi ya 300 zikitajwa kuzingirwa na maji na uwepo wa hatari ya kutokea kwa magonjwa ya mlipuko.

Athari nyingine zilizotokana na mvua hizo zimetajwa kuwa ni pamoja na barabara kujaa maji hali inayochangia wananchi wakiwemo wanafunzi kupata adha ya usafiri na hata kutembea kwa miguu na wengine kupoteza maisha.

Kutokana na hali hiyo serikali mkoani Kilimanjaro imezindua kamati ya Maafa ya mkoa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Sheria namba 7 ya mwaka 2015 ili kumshauri Mkuu wa mkoa kuhusu masuala ya usimamizi wa maafa na kuratibu shughuli za dharura miongoni mwa taasisi za kisekta za serikali za mitaa.

Wakichangia wakati wa kikao hicho kilichofanyika ukumbi mdogo wa ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, baadhi ya wajumbe wameeleza matarajio yao na namna ambavyo kamati hiyo inapaswa kutekeleza majukumu yake.

Kuzinduliwa kwa kamati hiyo kutasaidia upatikanaji wa rasilimali kwa ajili ya usimamizi wa maafa katika mkoa, kufungamanisha mfumo wa tahadhari ya awali katika mkoa na kuwezesha uanzishaji wa mfumo wa takwimu na taarifa za maafa za mkoa kwa kushirikiana na wakala.

Posted By

-

Leave a comment

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>