Published On: Thu, May 17th, 2018

MANYARA WATAKIWA KUSALIMISHA SILAHA

Share This
Tags

Mkuu wa Mkoa wa Manyara ALEXANDER MNYETI amewataka watu wote wanaomiliki silaha mkoani humo kuzisalimisha katika vituo vya polisi na kufanya utaratibu wa kuzisajili upya.

Amesema baadhi ya watu hutumia silaha hizo kufanya mauaji katika migogoro inayojitokeza ya mipaka kati ya wilaya ya Kiteto na Kilindi.

MNYETI amesema tayari ametoa maagizo kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara kufanya uhakiki wa silaha hizo ili kudumisha hali ya ulinzi na usalama hususan maeneo yenye migogoro.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga MARTIN SHIGELA akizungumza katika utatuzi wa Mgogoro  huo amesema kuna watu wanaomiliki silaha kiholela bila kufuata sheria na wamekuwa wakitumia silaha hizo kufanya uhalifu na kugharimu maisha ya watu, hivyo serikali haitawavumilia kwani hatua kali zitachukuliwa kwa watakao bainika.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi WILIAM LUKUVI amesema kuwa Wizara yake imeamua kutatua mgogoro huo kama Waziri Mkuu alivyoagiza hivyo wataweka alama za kitaalamu za nukta  zinazotambulika kimataifa zisizotumia vitu vinavyohamishika ili kuepusha migogoro kati ya wilaya hizo ikiwa ni pamoja na kuanisha mpango wa matumizi bora ya ardhi utakaosaidia kuepusha migongano isiyo na tija.

Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za mikoa na serikali za mitaa SULEIMAN JAFO amesema, kwa pamoja wamekubaliana na viongozi kumaliza mgogoro huo ambao umegharimu maisha ya watu wengi na kudumu kwa miaka mingi ili wananchi wajikite katika shughuli za kujiletea maendeleo.

Kwa upande wao Wananchi wa Wilaya ya Kiteto na Kilindi wamesema kutatuliwa kwa mgogoro huo kutasaidia kuepusha vitendo vya mauaji ya watu wasiokuwa na hatia ambavyo husababishwa na migogoro hiyo, hivyo wameiomba serikali iendeleze juhudi za kutatua migogoro katika maeneo mengi nchini.

Posted By

-

Leave a comment

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>