Published On: Wed, Apr 4th, 2018

Waziri Mkuu: Viwanda 3,306 vyaanzishwa nchini

Share This
Tags

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano imetekeleza kaulimbiu yake ya kujenga uchumi unaotegemea viwanda na kwamba hadi kufikia Februari 2018, viwanda vipya 3,306 vimekwishaanzishwa nchini.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Aprili 4, 2018) Bungeni mjini Dodoma, wakati akiwasilisha taarifa ya mapitio ya utekelezaji wa kazi za Serikali kwa mwaka 2017/2018 na mwelekeo wa kazi za Serikali kwa mwaka 2018/2019 kwenye mkutano wa 11 wa Bunge.

Amesema Serikali inahamasisha uwekezaji katika viwanda kwa kutoa vivutio vya kodi na visivyo vya kodi kwa wawekezaji mahiri (strategic investors); kuendeleza na kuboresha miundombimu wezeshi kama vile barabara, reli, bandari, umeme na maji. “Serikali itaendelea kuhuisha sera, sheria na kanuni pamoja na kufuatilia utendaji wa viwanda vilivyobinafsishwa na kuchukua hatua stahiki kwa wamiliki walioenda kinyume na mikataba ya mauzo,” amesema.

Waziri Mkuu amelieleza Bunge kwamba mikoa na Halmashauri zote nchini zimeelekezwa kutenga maeneo ya uwekezaji kwa ajili ya viwanda na kwamba katika mwaka 2018/2019, Serikali itatoa kipaumbele katika kutekeleza miradi ya kielelezo, uanzishwaji wa kanda maalum za kiuchumi pamoja na kuboresha mazingira ya biashara na kuvutia uwekezaji katika sekta ya viwanda.

Akitoa ufafanuzi kuhusu ushiriki wa sekta ya hifadhi ya jamii kwenye ujenzi wa uchumi wa viwanda, Waziri Mkuu amesema pamoja na miradi mingine NSSF na PPF kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza wanatekeleza mradi mkubwa wa uzalishaji wa sukari mkoani Morogoro.

“Lengo la mradi huo ni kuzalisha tani 250,000 za sukari na umeme megawati 40. Mradi huo unatekelezwa katika shamba la Mkulazi lililopo Ngerengere lenye ukubwa wa hekta 63,000 na shamba la gereza la Mbigiri lenye ukubwa wa ekari 12,000 lililopo Dakawa,” alisema.

“Hadi sasa ekari 2,000 za mashamba ya miwa zimetayarishwa katika eneo la Mkulazi na ekari 1,100 zimepandwa miwa. Lengo la Serikali ni kukamilisha awamu ya kwanza ya ufungaji wa mitambo ya kiwanda cha Mbigiri ifikapo mwezi Desemba, 2018 ili uzalishaji uanze mwaka 2019,” alisema na kuongeza kuwa miradi hiyo itakapokamilika, itazalisha zaidi ya ajira 100,000.

Waziri Mkuu alisema tangu kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo Juni 2017, ajira za moja kwa moja 780 na ajira zisizo za moja kwa moja  24,000 ikijumuisha wakulima wadogo wa mbegu na kilimo cha nje zimezalishwa.

Posted By

-

Leave a comment

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>