Published On: Tue, Apr 17th, 2018

Wakimbizi wahimizwa kurejea kwao

Share This
Tags

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga,  amewataka wakimbizi zaidi ya laki tatu kutoka Burundi walioko katika makambi ya Nyarugusu, Mtendeli na Nduta, kurejea kwao kwa kuwa sasa kuna amani na kwamba uwepo wao nchini umeendelea kuleta athari za kiusalama, kiuchumi na kiutamaduni katika jamii.

Brigedia Maganga, amesema hayo wilayani Kakonko mkoani Kigoma, muda mfupi baada ya kupokea Mwenge wa Uhuru kutoka mkoani Kagera, ambao utakimbizwa mkoani Kigoma kwa siku nane, kabla ya kukabidhiwa kwa mkoa wa Tabora.

Amesema suala la kuhifadhi wakimbizi linapaswa kufikia mwisho ili kutoa nafasi kwa wananchi wa mkoa wa Kigoma kufanya shughuli za maendeleo bila hofu na kwamba kwa sasa zoezi la kuhamasisha wakimbizi kurejea kwao limeanza.

Kwa upande wake kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu Charles Kabeho, akiongea baada ya kuzindua miradi kadhaa ya maendeleo ukiwemo mradi wa maji katika kijiji cha Kasanda uliofadhiliwa na taasisi ya Water Mission, amewataka wananchi kuitunza miradi hiyo.

Ukiwa mkoani Kigoma, Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika halmashauri nane, utatembelea miradi jumla ya miradi 50 yenye thamani ya takribani bilioni 12.9, ambapo kati ya miradi hiyo 24 itazinduliwa, 11 itafunguliwa, 11 itawekewa jiwe la msingi na miwili itakaguliwa.

Posted By

-

Leave a comment

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>