Published On: Wed, Apr 11th, 2018
Business | Post by jerome

Balozi wa Tanzania nchini DRC akutana na wafanyabiashara Kigoma

Share This
Tags

Wafanyabiashara kutoka Jimbo la Tanganyika nchini Congo DRC, na wafanyabiashara wa mkoa wa Kigoma upande wa Tanzania, wamesema urasimu na utitiri wa kodi katika bandari ya Kigoma na Kalemie, vimekuwa kikwazo cha biashara ya kuvuka mipaka kwa pande zote mbili.

Wafanyabiashara hao wamesema hayo mbele ya Balozi wa Tanzania nchini Congo Paul Ignace Mella, ambaye amefanya ziara mkoani Kigoma, akiambatana na waziri wa biashara, waziri wa uchukuzi wa jimbo la Tanganyika, pamoja na wawakilishi wa wafanyabiashara kutoka jimbo hilo.

Wakiongea katika kikao hicho ambacho mwenyeji wake alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, wafanyabiashara kutoka Congo DRC, wamesema kwa sasa wafanyabiashara ndogondogo ambao walikuwa wakifuata bidhaa Kariakoo Dar es Salaam, wengi wamehamia katika soko la Kampala nchini Uganda, kutokana na kero ambazo wamekuwa wakizipata upande wa Tanzania

Kwa upande wao Balozi Ignace Mella, na Waziri wa biashara jimbo la Tanganyika Musa Heri, wamesema changamoto hizo zitafikishwa katika mamlaka zinazohusika kwa hatua zaidi na kwamba nyingine zinazowezekana kutatuliwa kwenye mamlaka za chini zitatatuliwa.

Nae Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga, ametumia nafasi hiyo kuwahimiza wananchi wa Kigoma, kuona fursa iliyopo ya soko kubwa lililoko Mashariki ya Congo DRC, kwani zipo fursa nyingi za kibiashara.

Lengo la ziara hiyo ni kuona fursa na vikwazo vya kibiashara kwa wafanyabiashara wa mkoa wa Kigoma upande wa Tanzania, na wafanyabiashara kutoka jimbo la Tanganyika upande wa nchi ya Congo DRC, ili kuboresha mazingira ya biashara baina ya pande zote mbili.

Posted By

-

Leave a comment

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>