BALOZI WA TANZANIA NCHI ZA INDIA, NA SRI LANKA AWASILISHA HATI
Balozi wa Tanzania nchini India, Baraka Luvanda (kushoto) ambaye anawakilisha pia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kisoshalisti ya Sri Lanka amewasilisha Hati za Utambulisho kwa Maithripala Sirisena, Rais wa Nchi hiyo.
Hiyo ni hatua muhimu katika kuendeleza, kuimarisha na kukuza uhusiano wa kirafiki na ushirikiano mwema uliopo kati ya Tanzania na Sri Lanka ambao ulianza miaka ya 1990.
Wakati huo, Sri Lanka ilikuwa ikiwakilishwa nchini Tanzania kupitia Ubalozi wake wa mjini Kampala, Uganda ambao baadaye ulifungwa na Tanzania ikiwakilishwa nchini Sri Lanka kupitia Ubalozi wake wa New Delhi.
Kwa sasa Sri Lanka inakusudia kumteua Balozi wake mjini Nairobi ambaye pia ataiwakilisha nchi hiyo hapa nchini
Katika hafla hiyo, Balozi Luvanda aliambatana na Mwambata Jeshi wa Tanzania nchini India, Kanali Amri Salim Mwami.
Aidha, Balozi Luvanda alifanya mazungumzo na Mkuu wa Itifaki wa Sri Lanka pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Masuala ya Afrika, ambapo ameahidi kushirikiana kwa karibu na watendaji hao katika kudumisha uhusiano uliopo kati ya nchi hizi mbili.
Manufaa zaidi yanayotazamiwa na Nchi hizo ni katika kuhakikisha uhaulishaji wa uzoefu, teknolojia na utaalam wa Sri Lanka kwa Tanzania kwenye sekta ya viwanda vya nguo, madini na vito mbali mbali na kilimo.
Sri Lanka ni nchi yenye uchumi unaoendelea ingawa imepitia kipindi kigumu cha vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa takriban miaka 25, vita ambavyo vilimalizika mwaka 2009.