Published On: Tue, Mar 27th, 2018

JE KUNA HAJA YA KUPUNGUZA IDADI YA WACHEZAJI WA KIGENI KWENYE LIGI KUU TANZANIA BARA?

Share This
Tags

Na Heri Mijinga

Kwa miaka kadhaa idadi ya wachezaji wa kigeni katika ligi kuu Tanzania Bara (VPL) imekuwa ikileta gumzo  miongoni mwa wadau wa soka na mamlaka mbalimbali zinazohusika na mchezo wa soka nchini Tanzania. Mjadala mkubwa umekuwa kuongeza au kupunguza  idadi ya wachezaji wageni katika ligi kuu Tanzania Bara

#CloudsCheck imetafiti kwa kuzingatia maoni ya wadau na wachambuzi wa mchezo wa mpira wa miguu pamoja  na mifano kutoka kwenye ligi za nchi zingine za Afrika imebaini kuwa SI KWELI kwamba kuna haja ya kupunguza idadi ya wachezaji wa kigeni katika ligi kuu Tanzania Bara kwa sababu zifuatazo.

Miaka ya nyuma kumewahi kuwa na maazimio kadhaa yaliyolenga kupunguza idadi ya wachezaji wa kigeni, ikiwemo azimio la Bagamoyo (Bagamoyo Declaration) lililoazimiwa kuwa kuanzia msimu wa mwaka 2012-2013 kwa idadi ya wachezaji wa kigeni ipunguzwe hadi kufikia watatu angali

Mpango huo haukufanikiwa, uliondoka na uongozi  wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) uliokuwa chini ya Rais Leodgar Tenga. Uongozi uliofuata wa TFF chini ya Rais Jamal Malinzi kupitia kikao cha kamati ya utendaji kiliiagiza kurugenzi ya mashindano kufanya uchambuzi wa maoni ya vilabu juu ya idadi ya wachezaji wa kigeni.

Kutokana na shinikizo la vilabu vikubwa kama Azam FC, Simba SC na Yanga ambavyo ndivyo vilikuwa na wachezaji wengi wa kigeni, vilipambana kuhakikisha idadi ya wachezaji wa kigeni inaongezwa. Baadaye mwaka 2014 TFF iliweka kwenye kanuni zake na kuongeza idadi ya wachezaji wa kigeni kufikia saba.

Ukiachana na Tanzania ambayo kanuni zake zinatoa nafasi ya timu kusajili wachezaji wa kigeni wasiozidi saba, nchi zingine pia zinatofautiana, mfano; Afrika kusini (South Africa) inatoa ruhusa ya kusajili wachezaji watano huku Rwanda ikiwa ni wachezaji 3.

Baadhi ya mashabiki na wadau wa mpira wa miguu waliotoa maoni yao wameeleza kuwa kuna  haja ya kupunguza idadi ya wachezaji wa kigeni wanaocheza ligi kuu Tanzania Bara wakitoa sababu zifuatazo; Kwanza wameeleza uwepo wa wachezaji wengi  unawanyima nafasi wachezaji wazawa kuonyesha uwezo wao lakini pia wameeleza kuwa ni timu chache pekee ndizo zenye uwezo wa kusajili wachezaji wa nje wenye ubora na hivyo timu hizo ndizo zinatakazoendelea kufanya vizuri katika ligi kuu.

Mchambuzi wa soka James Samwel amefunguka na kutoa maoni yake akisema “hakuna haja ya kuwa na kanuni au sheria ya kuwa na kikomo cha idadi ya wachezaji wa kigeni kwa sasa kwa sababu moja, kuwepo cha idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni kunasaidia wachezaji wazawa kujitambua, pili kunaongeza ushindani kwenye soka kwa mechi za ndani na nje”

Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ilieleza kuwa  idadi ya wachezaji saba wa kigeni katika timu za soka za Ligi Kuu Tanzania Bara inatosha kwa sasa na hakuna sababu yoyote ya kuiongeza au kuipunguza.

Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) pia halina kikomo cha usajili ya wachezaji wageni kwenye timu ya ligi yoyote duniani, mashirikisho ya mpira wa miguu kwa nchi husika ndiyo yanayoweka mwongozo wa idadi ya wachezaji wa kigeni wanaotaka timu zao zisajili.

Kwa kuzingatia hayo ni wazi kuwa SI KWELI kwamba tunahitaji kupunguza idadi ya wachezaji wa kigeni katika vilabu vinavyoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) ili kuboresha timu ya taifa, uwekezaji thabiti na sera bora kwa soka la vijana ndio suluhisho la muda mrefu kwa maendeleo ya mpira wa miguu nchini.

Posted By

-

Leave a comment

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>