Published On: Tue, Feb 27th, 2018

JE, WATOTO TISA KATI YA KUMI WA KITANZANIA WANAPATA LISHE DUNI?

Na Belinda Japhet

Watoto wangapi walio chini ya umri wa miaka mitano wanapata lishe bora kwa kiwango wanachokihitaji?

Je, asilimia 92 ya watoto nchini Tanzania wanapata lishe duni?

Kwa mujibu wa Rikke Le Kirkegaard, mtaalamu wa masuala ya Afya anayefanya kazi na shirika la UNICEF jijini Dar es Salaam, ni asilimia nane tu ya watoto wa kitanzania wanapata kiwango cha chini cha lishe bora. Hii ina maana kuwa ni watoto 640,000 pekee kati ya watoto milioni 8 wenye chini ya miaka mitano walioko nchini, wanapata lishe bora.

Akitoa tathmini hiyo kutoka Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria 2015-16 Kirkegaard aliongeza kwa mtoto mmoja kati ya watatu wenye umri chini ya miaka mitano nchini Tanzania wamedumaa kwasababu ya kukosa virutubisho vya muhimu mwilini kama vitamini na madini, ambayo yanahitajika kwa ukuaji. Katika maeneo yaliyoathirika zaidi nchini, uwiano ni mkubwa zaidi, ambapo karibu mtoto mmoja kati ya wawili wameathirika.

Hali hii inafahamika kama “njaa iliyojificha”, ambapo aina ya chakula wanachokula watoto hakikidhi uhitaji wa virutubisho wanavyovihitaji, badala yake wanadumaa na kupata matatizo mengine kiafya hapo baadae.

Je, watoto wangapi Tanzania wanapata lishe bora kwa kiwango wanachokihitaji?

Uchunguzi uliofanywa juu ya madai anayoyasema Rikke Le Kirkegaard kuwa asilimia 8 tu ya watoto Tanzania wanapata lishe bora na umebaini kuwa jambo hili ni KWELI kwa sababu zifuatazo:

Shirika la Afya Duniani linafafanua kuwa utapiamlo ni upungufu, ziada, au kutokuwa na usawa katika kiwango cha chakula kinachompa mtu nguvu au virutubisho mwilini. Hali hii inaangalia makundi mawili, kwanza, kutokuwa na lishe ya kutosha ambako kunajumuisha kudumaa, kuwa na uzito mdogo pamoja na kukosa virutubisho vya kutosha. Pili, kula vyakula vinavyoleta unene uliopitiliza na magonjwa yanayotokana na mtindo wa maisha.

Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria 2015-16, ni asilimia 9 tu ya watoto wa kitanzania wenye umri wa kati ya miezi 6 na miaka 2 wanaopata kiwango cha chini cha lishe kinachohitajika, huku asilimia 4 ya watoto wasionyonyeshwa wakipata kiwango cha chini zaidi.

Muhtasari wa hali ya utapiamlo Tanzania ya mwaka 2016 unaweka mambo katika muktadha sahihi kwa kuonyesha kuwa asilimia 34 ya watoto chini ya umri wa miaka mitano nchini, asilimia 25 mijini na asilimia 38 vijijini wamedumaa.

Kinachosababisha tatizo kuwa kubwa kwa kiwango hiki ni  watoto kutopata mlo kamili katika kaya nyingi zilizoko mijini. Watu wengi hula vyakula vya wanga kwa wingi, kwa mfano, ugali ambao unapikwa kwa kutumia unga wa mahindi, unga wa mtama au muhogo, pia mchele, na vyakula vya jamii ya maharage. Milo mingi hukosa mchanganyiko wa protini ya wanyama na mimea, mbogamboga na matunda.

Hata hivyo, utapiamlo kwa watoto nchini Tanzania unapungua. Ripoti ya UNICEF iliyoangalia viwango vya ukosefu wa lishe kati ya mwaka 1992 – 2015 inaonyesha kwamba nchi imefanya jitihada za kutosha kukabiliana na utapiamlo:

“Kumekuwa na maendeleo mazuri katika jitihada za kuboresha hali ya lishe kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano kati ya mwaka 1992 na 2015. Kudumaa na utapiamlo sugu kumepungua kutoka asilimia 50 hadi 34, huku utapiamlo uliokithiri ukipungua kutoka asilimia 7 hadi 5, na hali ya upungufu wa uzito ukipungua toka asilimia 24 hadi 14” UNICEF Tanzania

 

Takwimu alizotoa Le Kirkegaard zinaonesha kuwa ni asilimia 8 ya watoto wa kitanzania wanaopata kiwango cha chini cha lishe inayohitajika, lakini kwa uhalisia ni asilimia 9. Kiwango kimeshuka kutoka ilivyokuwa mwaka 2014 ambapo utafiti wa UNICEF ulionesha kuwa asilimia 20 ya watoto wa kitanzania kati ya miezi 6 na miaka 2 walikuwa wanapata lishe ya kutosha.

Ripoti ya Twaweza inaonesha kuwa hali ilikuwa mbaya zaidi baada ya kuwa na upungufu wa chakula, ambapo mwanzoni mwa mwaka 2017, takriban asilimia 51 ya kaya nchi nzima ziliripotiwa kutokuwa na chakula cha kutosha. Uhaba huu wa chakula ulisababisha kupanda kwa bei ya chakula, ukifanya iwe vigumu kwa watu masikini kupata chakula cha kutosha na vyakula vya aina mbalimbali ili kupata mlo kamili.

Hivyo, alichosema Le Kirkegaard kuwa asilimia 8 tu ya watoto wa kitanzania wanapata kiwango cha chini cha lishe inayohitajika, ni KWELI.

 

 

 

Posted By

-

Leave a comment

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>