Published On: Tue, Feb 27th, 2018

JE NI SAHIHI MAGARI BINAFSI KUTUMIA VITUO VYA DALADALA?

Share This
Tags

Katika siku za karibuni kumekuwa na taarifa iliyokuwa ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii ikieleza kuwa magari binafsi hayaruhusiwi kushusha abiria katika vituo vya basi maarufu kama vituo vya daladala. Taarifa hiyo ilieleza kuwa endapo gari binafsi likikamatwa, basi hatua za kisheria zingechukuliwa juu yake ikiwemo kulipa faini.

Sintofahamu hii ilikuwa kubwa na kusambaa kwa haraka sana hasa katika mtandao wa kutumiana ujumbe wa maandishi (SMS) wa “Whatsapp” pamoja na mitandao mingine kama “Facebook” na “Twitter”.

Ujumbe huo unaeleza kuwa kwa mujibu wa sheria ni mabasi ya abiria pekee yanaruhusiwa kuegeshwa katika vituo hivyo kwa lengo kushusha au kupandisha abiria na endapo gari lingine lolote la binafsi likifanya hivyo basi limekiuka sheria.

WANANCHI WANASEMAJE?

Wananchi wengi waliochangia mjadala huu katika mitandao mbalimbali ya kijamii wameonyesha kwanza kutokuridhika na hatua hiyo huku wakihoji ni wapi basi wanapaswa kushusha abiria wanapokuwa barabarani lakini pia wameonyesha sintofahamu na uelewa mdogo juu ya nini hasa sheria na wasimamia sheria wanasema juu ya magari binafsi kushusha abiria katika vituo vya mabasi.

#CloudsCheck imefanya ufuatiliaji juu ya sintofahamu ili kupata hali halisi kwa lengo la kuondoa mkanganyiko uliopo ambapo imegundua kupishana kwa tamko la jeshi la polisi pamoja na kile kinachosemwa na sheria husika.

SHERIA INASEMAJE

Watumiaji wa barabara nchini Tanzania wanaongozwa na sheria ya usalama barabarani ya mwaka 1973 inayotoa miongozo kadhaa ya matumizi sahihi ya barabara. Matumizi ya barabara yanaongozwa na alama za barabara ambazo zimegawanywa katika makundi matatu, alama za kudhibiti (katazo), alama za tahadhari na alama za taarifa.

Alama inayoonyesha uwepo wa kituo cha mabasi ni alama iliyo katika kundi la alama za taarifa ambapo humwarifu mtumiaji wa barabara juu ya uwepo wa kituo cha mabasi.

Kwa mujibu wa sheria ya usalama barabarani ya mwaka 1973, kifungu cha 71A(3)(c) inaeleza wazi kuwa “hakuna dereva atakayeruhusiwa kuegesha gari barabarani katika kituo cha basi au mita 15 ya kila upande wa alama ya kituo cha basi (bus stop sign)”.

MAMLAKA ZINASEMAJE?

Baada ya kusambaa kwa taarifa hizi kwa kiasi kikubwa,Jeshi la Polisi kupitia kwa Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama barabarani, Fortunatus Muslimu walitoa taarifa kufafanua juu ya taarifa hizi ambapo, Kamanda Muslimu alieleza kuwa taarifa inayosambazwa  kwenye mitandao ya kijamii kuwa, magari binafsi hayatakiwi kushusha watu kwenye vituo vya daladala siyo sahihi, na amewataka wananchi kuipuuza

NINI KIFANYIKE?

Kwa kuwa sheria ya usalama barabarani ya mwaka 1973 inaeleza wazi kuwa hairuhusiwi magari binafsi kuegesha katika vituo vya daladala.

Na kwa kuwa sheria hiyohiyo kifungu cha 72 inaeleza kuwa Waziri mwenye dhamana ya usalama barabarani anapaswa kutenga maeneo ambayo yatakuwa maegesho kwa ajili ya magari binafsi, kwa kufanya hivyo ni dhahiri kuwa mosi mamlaka husika hazina budi kutoa maelezo ya kina hasa kwa kuzingatia tamko la sheria na sio kutoa majibu ya ujumla yanayoacha maswali zaidi miongoni mwa wananchi.

Pili kama sheria inavyoelekeza Waziri mwenye dhamana atenge maeneo kwa ajili ya magari binafsi na maeneo hayo yawekwe wazi lakini pia kwa umuhimu mkubwa mabadiliko ya sheria yafanyike kuendana na nyakati ili kuruhusu magari binafsi kutumia vituo vya daladala kwani ni dhahiri idadi ya magari binafsi imeongezeka sana tofauti na kipindi ambacho sheria hiyo ilitungwa

Posted By

-

Leave a comment

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>