Published On: Wed, Jan 31st, 2018

Rais Magufuli azindua mfumo wa uhamiaji mtandao

Share This
Tags

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo amezindua mfumo wa uhamiaji mtandao (e-Immigration) ambao utasaidia kuimarisha ulinzi na usalama wa mipaka ya nchi, kudhibiti ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali na kuimarisha utoaji wa huduma za kiuhamiaji kwa raia wa Tanzania na wageni wanaoingia na kuishi hapa nchini kwa madhumuni mbalimbali.

Uzinduzi wa mfumo huo umefanyika katika ofisi kuu ya uhamiaji Jijini Dar es salaam na kuhudhuriwa na Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein,Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Seif Ali Iddi, na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa.

Wengine ni Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Hamis Juma, Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson Mwansasu, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Dkt. Ali Hassan Mwinyi na Rais Mstaafu wa Zanzibar Amani Abeid Karume.

Kabla ya kuzindua mfumo wa uhamiaji mtandao Rais Magufuli amekagua teknolojia iliyotumika katika mfumo huo ikiwa ni pamoja na kuchukuliwa alama za vidole na baadaye kupatiwa pasipoti mpya ya kielekektronikia (e-Passport) ambayo pia imeanza kutolewa leo.

Rais Magufuli amempongeza Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba na Idara ya Uhamiaji kwa kufanikisha mchakato uliofanikisha uwepo wa mfumo wa uhamiaji mtandao na kuanza kutoa paspoti mpya ya kielektronikia kwa gharama nafuu ya Shilingi Bilioni 127.2 ikilinganishwa na makadirio yaliyowekwa awali ya Shilingi Bilioni 400.

Mapema akitoa taarifa ya mfumo wa uhamiaji mtandao, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala amesema mfumo huo ni muunganiko wa mifumo mbalimbali ambayo imesanifiwa kufanya kazi kwa pamoja, kutoa taarifa kwa watumiaji na wadau wa huduma za kiuhamiaji na kwamba kupitia mfumo huo idara ya uhamiaji inatarajia kutoa paspoti za kielektronikia (e-Passport), viza za kielektronikia (e-Visa), vibali vya ukaazi vya kielektronikia (e-Permit) na udhibiti wa mipaka wa kielektronikia (e-Border Management) kwa awamu nne hadi ifikapo mwisho wa mwaka huu 2018, pamoja na kutoa paspoti ya kielektronikia ya Afrika Mashariki ya Tanzania.

Balozi wa Ireland hapa nchini Paul Sherlock ameipongeza Tanzania kwa kufanikisha mradi huu na kueleza kuwa mfumo huu wa uhamiaji mtandao ni alama muhimu ya Taifa.

 

Posted By

-

Leave a comment

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>