Published On: Sat, Dec 16th, 2017

Weledi na Ubora wa Kazi Ndio Msingi Mzuri wa Kupata Soko la Sanaa- Dkt. Mwakyembe.

Share This
Tags

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe amewataka Wasanii wote hapa Nchini kuwa wabunifu na kutumia weledi katika kutengeneza kazi zenye ubora wa hali ya juu kwakua ndio utakaowasaidia kupata soko la uhakika.

Dkt. Mwakyembe ameyasema hayo leo Jijini Dar es Salaam wakati akizindua Kanzi Data ya wasanii iliyoandaliwa na Taasisi ya Muziki hapa nchini (TAMUF) iliyodhaminiwa na Kampuni ya CogsNet Technologies lengo ikiwa ni kusajili wasanii pamoja na kazi zao ili watambulike na wafaidike  kupitia kazi hizo, lakini pia kuendelea na harakati za kupambana na wizi wa kazi za wasanii.

“Nawashukuru sana CogsNet pamoja na TAMUF kwa kuja na wazo hili lenye lengo la kulinda kazi za wasanii,naamini Kanzi Data hii italeta mafanikio kwa wasanii endapo watajisajili na kutengeneza kanzi bora zitakazowapatia soko la uhakika ndani na nje ya nchi”Alisema Dkt.Mwakyembe.

Aidha ameipongeza Taasisi hiyo kwa kuwatafutia wasanii Huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo Bima ya Afya inayotolea na mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa NSSF lengo ikiwa ni kuwasaidia wasanii kupata huduma ya afya kwa bei nafuu pamoja na mafao mengine yanayotolewa na Mfuko huo lakini pia akiwataka wasanii kuacha tabia ya kuuza Haki Miliki zao.

Kwa upande wake Rais wa Taasisi hiyo Dkt.Dornald Kisanga amesema kuwa Taasisi hiyo ina lengo la kuondoa unyanyasaji wa kazi za wasanii uliofanywa kwa muda mrefu  ikiwemo wizi wa kazi hizo pamoja na kipato kidogo walichokuwa wanapata wasanii kwa kuuza Haki Miliki zao.

“Kumekuwa na changamoto ya muda mrefu ya wizi wa kazi za wasanii ndio maana CogsNet Technologies imeamua kushirikiana nasi katika kutafuta suluhu ya kazi ya kunufaika na kazi zetu,hivyo wasanii tunapaswa kutumia nafasi hii kwa manufaa yetu”Alisema Bw.Kisanga.

Naye mwakilishi wa NSSF Omary Mzia amesema mpaka sasa wasanii 500 wameandikiswa katika mfuko huo ili kupata huduma mbalimbali za hifadhi ya jamii ambapo amewakaribisha wasanii wengine kujiunga na mfuko huu ili wapate huduma zinazotolewa na mfuko huo ikiwa ni pamoja na huduma ya matibabu.

Hata hivyo muwakilish wa wasanii kutoka Taasisi hiyo ya TAMUF Bibi Leonia Leornad ameishukuru Serikali kwa kuunga mkono hatua zinazofanywa na Taasisi yao katika kuhakikisha wasanii wananufaika na kazi zao kwa kupiga vita wizi wa kazi hizo pamoja na kuishukuru NSSF kwa kuwapatia huduma ya matibabu.

Taasisi ya TAMUF imeahidi kutoa elimu kwa wasanii kutengeneza nyimbo pamoja na video zinazozingatia maadili na Utamaduni wa Watanzania ikiwa ni kuunga mkono jitihada za Serikali za kukomesha kazi za sanaa zisizozingatia maadili.

 

Posted By

-

Leave a comment

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>