Published On: Wed, Nov 29th, 2017

Waziri mkuu amkabidhi IGP waliotaka kutoa semi tela 44 bila kukamilisha taratibu

Share This
Tags

 

Waziri mkuu Kassim Majaliwa amemtaka Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro kuwakamata,. Bahman wa kampuni ya NAS na Wakala wa Kampuni ya Wallmark Samwel kwa kutaka kutoa bandarini magari makubwa aina ya semi tela 44 bila ya kulipa kodi kwa kutumia jina la Waziri Mkuu.

Pia Waziri Mkuu ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na kutowasikiliza wafanyabiashara wanaotaka kukwepa kodi kwa madai ya kupewa vibali vya msamaha wa kodi kutoka kwa viongozi wa juu Serikalini.

“Mtu asije hapa aseme amepewa kibali na Rais Dkt. John Magufuli, Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan au Waziri Mkuu cha kutaka kutoa mzigo wake bila ya kufuata taratibu. Akija mtu na taarifa hizo akamatwe mara moja na achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.”

Ametoa agizo hilo leo alipofanya ziara ya ghafla bandarini baada ya kupata taarifa za mfanyabiashara huyo aliyetaka kuutapeli uongozi wa TPA kutaka kutoa magari hayo yaliyoingizwa nchini mwaka 2015 kutoka nchini Uturuki.

Hatua hiyo imekuja baada ya Bw. Bahman wa kampuni ya NAS kutaka kupata msamaha wa  kodi kwa kuidanganya TPA kwa madai kwamba wamewasiliana na Waziri Mkuu na wasipotekeleza jambo hilo watapata matatizo.

Amesema Serikali inasisitiza watu kufuata sheria na taratibu za nchi ikiwa ni pamoja na kulipakodi  ipasavyo na inataka watendaji wake wafanye kazi bila ya kubugudhiwa, hivyo amewataka wafanyabiashara kufuata sharia za nchi na kwamba Serikali haina ugomvi nao.

Waziri Mkuu amefafanua kuwa mfanyabiashara huyo alitaka kuyatoa magari hayo bila ya kukamilisha malipo ya ununuzi kutoka kwenye kampuni Serin ya nchini Uturuki.

Waziri Mkuu pia ametoa wito kwa Mawakala wa Forodha kuhakikisha wanakuwa makini katika kazi zao na Serikali haitawavumilia wababaishaji kwani inasisitiza wafanyabiashara kulipa kodi kwa mujibu wa sheria na si vinginevyo.

Awali, Mkurugenzi wa Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko alimueleza Waziri Mkuu kuwa pamoja na vitisho vya mfanyabiashara huyo kuwa wasipotekeleza matakwa yake watapata matatizo, lakini waliendelea kusimamia sheria na taratibu.

Posted By

-

Leave a comment

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>