Published On: Wed, Nov 22nd, 2017

Naibu waziri wa maliasili na utalii, aagiza kuundwa kwa chombo cha kudhibiti ubora wa mazao ya misitu.

Share This
Tags

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga ameuagiza uongozi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kubuni utaratibu mpya ikiwemo kuanzishwa kwa chombo kitakachosimamia upangaji wa madaraja ya ubora wa mbao zinazozalishwa hapa nchini ziweze kukidhi viwango vya mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi.

Ametoa agizo hilo kwenye kikao cha majumuisho na watumishi wa Shamba la Miti la Serikali la Kiwira ambalo linasimamiwa na wakala huyo wakati anahitimisha ziara yake ya kikazi ya siku moja katika Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya.

Hasunga amesema amepata taarifa kuwa baadhi ya wananchi wanavuna miti ambayo haijakomaa jambo ambalo linaathiri ubora wa mbao kwenye soko kwa kutokidhi mahitaji ya wateja, hivyo akaagiza Wakala huyo kubuni mbinu mpya za kuwalinda wateja ikiwemo kuanzishwa kwa chombo maalum cha udhibiti wa ubora wake.

Aidha ametoa wito kwa taasisi hiyo kuendelea kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kuvuna miti ikiwa imeshakomaa pamoja na kuongeza uzalishaji wa miche ya miti na kuhamasisha wananchi wapande miti zaidi kwa faida yao na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wa kampeni ya upandaji miti kitaifa, naibu waziri huyo amesema Serikali itafuatilia nchi nzima kuona utekelezaji wa agizo hilo ambalo linaitaka kila Wilaya kupanda miti milioni moja na laki tano kwa mwaka ikiwa ni pamoja na kuweka mikakati ya pamoja ya kuhakikisha miti mingi zaidi inapandwa kwa kuwashirikisha zaidi wananchi.

 

Awali Meneja wa Shamba la Miti Kiwira William Dafa, akiwasilisha taarifa yake kwa Naibu Waziri Hasunga, amesema shamba hilo ambalo lilianzishwa mwaka 1964 likiwa na hekta 2,713 limekuwa na maendeleo mazuri ambapo mwaka 2016/2017 lilivuka malengo ya makusanyo ya mapato ya Serikali kutoka bilioni 1.3 hadi bilioni 1.7.

Posted By

-

Leave a comment

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>