Published On: Tue, Sep 12th, 2017

Taasisi za serikali zatakiwa kutatua kero za wananchi kwa vitendo

Share This
Tags

Serikali mkoani Iringa imeziagiza taasisi zake zote zinazotoa huduma kwa wananchi kutenga muda usiopungua masaa sita kwa siku ya Jumatatu ili kupokea na kutatua kero za wananchi zinazotokana na kutoridhishwa na huduma zinaotolewa na Taasisi hizo.

Agizo hilo limetolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa Amina Masenza kufuatia utitiri wa wananchi wanaofika ofisini kwake kupeleka malalamiko ya kutoridhishwa na huduma zinazotolewa na taasisi za serikali jambo linalochangia wananchi kuijengea chuki Serikali.

Kufuatia agizo hilo  mkuu huyo wa mkoa amefanya ziara katika baadhi ya taasisi hizo ikiwemo Shirika la Umeme nchini TANESCO,Mamlaka ya Maji safi mjini Iringa IRUWASA,Mamlaka ya Mapato Tanzania mkoani Iringa pamoja na ofisi ya mkuu wa wilaya ya Iringa ili kukagua namna wanavyotekeleza agizo hilo kwa vitendo na kuzitaka taasisi ambazo bado zinasusua kuongeza juhudi ya kusikiliza malalamiko ya wananchi na kuyatafutia ufumbuzi.

Aidha Masenza ametoa wito kwa Taasisi za serikali kutimiza majukumu yao katika kushughulikia changamoto za wananchi ili kuweza kupata majibu ya kero zao huku akionesha kutoridhishwa na utekelezaji wa agizo hilo katika Shirika la Umeme  TANESCO na Mamlaka ya Mapato mkoani Iringa TRA.

Gribat Kayange ni mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safia na Usafi wa Mazingira Mkoani Iringa akitoa Taarifa ya utekerezaji wa agizo hilo amesema Tayari mamlaka hiyo imetatua kero  71 kati ya wananchi 79 waliokutana nao jambo linaloashiria mafanikio makubwa katika kupunguza adha kwa wananchi badala ya kuwaacha wakihangaika kutafuta ofisi ya mkuu wa mkoa ili kupeleka malalamiko yao.

Kwa upande wake Meneja wa TANESCO Iringa Mhandisi  Selafin Lyimo amesema Shirika hilo limetenga siku mbili katika wiki ili kushughulikia kero za wateja wao ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Agizo la mkuu wa Mkoa wa Iringa ambapo kupitia dawati hilo kero mbalimbali zinatatuliwa na kuendelea kupunguza Usumbufu kwa wananchi waliokuwa wakiupata awali.

Imeelezwa kuwa zoezi hilo la usikilizwaji wa kero za wananchi na kuzitatua limesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza foleni na malalamiko yanayotokana na kukaa muda mrefu pasipo kupatiwa huduma wala kusikilizwa jambo lililochochea chuki kwa serikali.

 

Posted By

-

Leave a comment

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>