Published On: Sat, Aug 12th, 2017

Waziri mkuu akemea maafisa misitu

Share This
Tags

Waziri mkuu Kassim Majaliwa amekemea tabia ya kutoa vibali vya uvunaji mbao inayofanywa na maafisa misitu wa TFS ambao wako chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

Ametoa onyo hilo leo wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui kwenye mkutano uliofanyika kata ya Goweko, wilayani Uyui mkoani Tabora.

Waziri Mkuu alifikia hatua hiyo baada ya kumhoji Afisa Misitu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Juma Kazimoto na Afisa Misitu wa Wilaya Jared Nzilorera na kubaini kuwa hawafanyi kazi kwa kushirikiana.

Akijibu swali la Waziri Mkuu  Kazimoto alisema Uyui hakuna uvunaji lakini wanaovuna wanatoka Sikonge na kuja kuuza mbao Uyui.

Alipoulizwa Afisa Misitu wa Wilaya,  ni kwa kiasi gani wanapeana taarifa na mwenzake wa TFS ambao wanaletwa na wizara, alitoa majibu ya kujichanganya hali iliyomfanya Waziri Mkuu aamue kukemea tabia yao ya kutoa vibali bila kuwahusisha wenzao wa Halmashauri.

Aidha waziri mkuu akamuagiza Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Uyui, Bi. Queen Mlozi asimamie suala hilo.

Amesema ukataji miti ovyo umechangia kukauka kwa vyanzo vingi vya maji. “Mhandisi wa Maji anahangaika kuchimba visima lakini hakuti maji sababu miti imekatwa ovyo na ardhi tepetevu imekauka. Watumishi wote nendeni vijijini mkahamasishe utunzaji wa mazingira,” alisema.

Kwa mujibu wa hali ilivyo sasa, kila mkoa una Afisa Misitu wa Mkoa, kila wilaya imeajiri Afisa Misitu wa Halmashauri, lakini Wizara pia imeajiri Maafisa wa Misitu kutoka TFS katika ngazi za mkoa na wilaya.

Posted By

-

Leave a comment

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>