Published On: Tue, Aug 1st, 2017

Mambo kumi yasiyofaa kukupita kuhusu uchaguzi mkuu Kenya 2017

Share This
Tags

Kwa mara nyingine tena, Uhuru Kenyatta na Raila Odinga, wanashindania uongozi wa taifa la Kenya katika uchaguzi wa Agosti baada ya kukabiliana tena Machi 2013.

Rais Kenyatta ni mwana wa rais wa kwanza wa Kenya, Mzee Jomo Kenyatta naye Bw Odinga mwana wa makamu wa rais wa kwanza Jaramogi Oginga Odinga.

Uchaguzi wenyewe, kuanzia kipindi cha kabla ya kampeni, umeshuhudia mambo ya kipekee. Tumekusanya baadhi hapa:

1) Kuna farasi, punda, mbuni na ngamia

Kinyang’anyiro cha urais kimewavutia wagombea wanane, Uhuru Kenyatta wa Jubilee, Raila Odinga wa Nasa, Cyrus Jirongo wa United Democratic Party (UDP), Ekuru Aukot wa Thirdway Alliance, Abduba Dida wa Alliance for Real Change (ARC), na wagombea huru Joseph Nyagah, Michael Wainaina na Japheth Kavinga.

Wachanganuzi wanasema ushindani mkali sana ni kati ya Bw Odinga na Bw Kenyatta na hivyo tamko la mbio za farasi wawili limekuwepo, yaani ‘Two horse race’.

Wagombea wengine kwa kukerwa na hili nao wamejipa majina yao ya utani. Bw Nyagah, ambaye jina lake maana yake ni mbuni ameamua kujiita ‘Mbuni’, ndege ambaye ana kasi sana ardhini. Bw Aukot, anayetoka eneo la Turkana, kaskazini magharibi mwa Kenya ambapo kuligunduliwa mafuta, na kuna kisima kifahamikacho kama Ngamia, amejiita Ngamia.

Bw Kaluyu naye amejiita punda, ambaye yuko tayari kubeba mizigo ya wananchi. Viongozi wa upinzani katika mikutano ya hadhara, wamekuwa mara kwa mara wakisema ‘Punda Amechoka’, kwa maana ya wananchi wamechoshwa na utawala mbaya. Dkt Kaluyu anasema yeye ni punda na raia ni punda wenzake.

2) ‘Yaliyo Ndwele Sipite’

Yaliyopita si ndwele, tuyagange yajayo. Wengi wanaifahamu methali hii ya Kiswahili. Lakini mgombea wadhifa wa ugavana katika jimbo la Machakos kwa tiketi ya chama cha Wiper kilicho kwenye muungano wa NASA alipokuwa anawahutubia wanahabari, yamkini ulimi uliteleza. Alisema ‘Yaliyo ndwele sipite’ badala yake.

Wakenya walianza utani mtandaoni na ghafla kukawa na Shindano la Wavinya.

Wakenya walikuwa wanashindana kutunga methali za Kiswahili kwa kuufuata ulimi wa Wavinya ulioteleza.

Mfano, badala ya Mtoto wa nyoka ni nyoka, Nyoka na mtoto wake ni nyoka. Badala ya Mwenda tezi na omo marejeo ni ngamani, unapata Mwenda tezi na ngamani marejeo ni omo. Haraka haraka haina baraka inakuwa Baraka baraka haina haraka.

Wengi walifurahia sana utani huo na mchekeshaji MC Njagi akatumia fursa hiyo kutunga wimbo wa utani kwa jina Yaliyo Ndwele Sipite ambao nao pia ulivuma.

Chama cha Jubilee kilitambua ufanisi wa wimbo huo na kumuomba MC Njagi atunge wimbo wa kusifu chama hicho.

Baadaye, MC Njagi pia alitunga wimbo pia wa kumuunga mkono mgombea huyo ambaye ni wa muungano wa Nasa.

3). Safari ya kwenda Canaan

Ukafika Kenya kwa sasa, unaweza kuwasikia baadhi ya wananchi wakizungumzia kuhusu safari ya kwenda ‘nchi ya ahadi’ – Canaan.

Mbona Wakenya watake kwenda Israel?

Yote yalianza mgombea wa Nasa Raila Odinga alipotangaza kwamba yeye atakuwa kama Joshua anayetajwa kwenye Biblia ambaye aliwavusha wana wa Israeli hadi nchi ya ahadi.

Bw Odinga alitangaza kuwa angekuwa kiongozi wa mpito iwapo atachaguliwa kuongoza Kenya.

„Tumekuwa na vikao ambavyo vimechukua siku nyingi. Kila kitu tumeandika, tumekubaliana ya kwanza serikali tutakayoiunda, ambayo ni serikali ya mseto itakuwa ni serikali ya mpito,” alisema baada ya kuidhinishwa kuwa mgombea.

Muungano wa Nasa ulianza kuvumisha dhana kwamba ndio muungano unaowapeleka Wakenya nchi ya ahadi Caanan.

Wakenya mtandaoni pia wamekumbatia wazo hilo na kuanza kulifanyia utani mitandao ya kijamii. Kwa kuchukulia safari hiyo kuwa ya kweli, wanajadiliana kuhusu vitu wanavyohitaji kwa safari hiyo, na watu watakaowakuta huko.

Bw Odinga pia hajaachwa nyuma, mfano leo amewasalimia watu na kuwaita ‘Watu wa Canaan’.

Posted By

-

Leave a comment

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>