Published On: Fri, Aug 4th, 2017

HUDUMA ZA AFYA ZASIMAMA KWA KUKOSA MAJI KIGOMA

Share This
Tags

Huduma za upasuaji katika kituo cha afya cha Bitale, kilichoko wilayani Kigoma, zinalazimika kusimama mara kwa mara kutokana na kituo hicho kukosa huduma ya maji kwa takribani mwezi mmoja hivi sasa.

Mganga Mfawidhi wa kituo hicho, Dr. Norbert Nshemetse, amesema kukosekana kwa huduma ya maji kumetokana na kuharibika kwa miundombinu ya maji katika kijiji cha Bitale, hivyo baadhi ya huduma kama za maabara na upasuaji zimelazimika kusimama kwa sababu hakuna maji ya uhakika.

Amesema angalau kwa siku mbili zilizopita wameweza kusaidiwa kupelekewa maji na kikosi cha jeshi la zimamoto mkoani Kigoma, lakini msaada huo hautakuwa endelevu hivyo ni muhimu hatua madhubuti zichukuliwe ili huduma hizo ziendelee kutolewa.

 

Tatizo la maji halijaathiri kituo cha afya pekee bali wananchi wote wa kijiji cha Bitale, ambao kwa sasa wanatumia maji yaliyotuama kwenye vidimbwi na mto ambapo Afisa Afya wa Kata ya Bitale, Kisela Leonard, amesema wanapata changamoto katika kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kuchemsha maji huku baadhi ya wananchi waliofika kituo cha afya cha Bitale, wakielezea adha ya maji.

Diwani wa Kata ya Bitale, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, Mathias Bwami, amesema tatizo la maji limevikumba vijiji tisa ambavyo vyote vilikuwa vinategemea maji ya chanzo cha mto Mkongoro ambacho kwa sasa kimeharibika.

Posted By

-

Leave a comment

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>