Published On: Mon, Jun 19th, 2017

WALALAMIKIA BOMOABOMOA KIGOMA

Share This
Tags

Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini, imeanza kubomoa nyumba za wakazi wa Majengo Kata ya Machinjioni Manispaa ya Kigoma Ujiji, ili kuruhusu maandalizi ya upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Kigoma ambacho ujenzi wake unatarajiwa kuanza mapema mwakani.

Hata hivyo hatua hiyo imelaumiwa vikali na wakazi wa maeneo hayo ambao wengi wamebaki bila makazi huku wakidai kunyonywa haki yao kwa kulipwa pesa kidogo isiyolingana na thamani halisi ya nyumba zao.

Mwezi Machi mwaka huu wakazi hao walipewa notisi ya kuondoka katika maeneo hayo lakini wengi hawakuondoka wakisubiri kulipwa malipo ya pili ya shilingi laki tano kila mmoja ambayo serikali iliahidi kuwalipa baada ya kulalamika kuwa fidia ya awali ilikuwa kidogo, lakini wameshangaa kubomolewa nyumba zao kabla ya kulipwa pesa hiyo.

Katika hatua nyingine wananchi hao ambao wengi wao ni waumini wa dini ya kiislam, wamelaumu kushtukizwa na bomoa bomoa hiyo huku mamlaka ikijua wazi kuwa hiki ni kipindi cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, hivyo kuharibiwa funga zao.

Takribani nyumba 300 zilizo katika mitaa ya Ukumbi, Kitenge, Wakuha na Kirugu katika Kata ya Machinjioni, zitakumbwa na bomoa bomoa hiyo huku wananchi hao wakisisitiza serikali iangalie suala hilo kwa kuwa sio haki kulipwa fidia mwaka 2013 kwa tathimini iliyofanywa mwaka 2008.

Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Kigoma, Mohamed Issa, amesema uamuzi wa kubomoa nyumba hizo umefuata sheria kwa kuwa malipo yao ya msingi walishalipwa na kwamba nyongeza ya shilingi laki tano ni huruma ya serikali ambayo itabidi wakazi hao wasubiri.

Upanuzi wa kiwanja cha ndege cha kigoma ambao ukikamilika utawezesha ndege kubwa aina ya Boeing 737, kutua na kukifanya kiwanja hicho kuwa na hadhi ya kimataifa unatarajiwa kuanza wakati wowote mwakani.

 

Posted By

-

Leave a comment

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>