Published On: Fri, Jun 16th, 2017

PROF: PATRICK LUMUMBA NDANI YA KIGODA CHA NYERERE

Share This
Tags

 

Mwanasheria msomi na nguli nchini Kenya, Prof PATRICK LUMUMBA ameeleza kuwa siasa chafu zinazofanywa na baadhi ya Viongozi wa Bara la Afrika, zimesababisha Mataifa mengi Barani humo, kutopiga hatua kimaendeleo.

Prof PATRICK LUMUMBA Mwanasheria nguli nchini Kenya ameonyesha kuguswa na kumfananisha Rais DK JOHN POMBE MAGUFULI na baadhi ya Viongozi wa Afrika wanaoheshimika kwa kutolea mfano kwa kuigiza makubaliano yaliyofikiwa baina yake na Mwenyekiti wa Mgodi wa Barrik.

Amesema kwamba kutokana na juhudi anazozifanya, katika miaka 10 ijayo Tanzania itakuwa na nafasi nzuri kiuchumi, lakini akamtahadharisha asilewe sifa.

Profesa Lumumba alikuwa akizungumza jana wakati wa kongamano la tisa la Kigoda cha Mwalimu Nyerere lililofanyika katika Ukumbi wa Nkrumah wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

“Najua baadhi ya Watanzania wanaweza kudhani nina ajenda fulani, mimi si mwana CCM ila kuna msemo unasema mgema akisifiwa tembo hulitia maji. Kwa hiyo, naamini Magufuli atabaki kwenye njia kuu na hatachepuka, Mungu amlinde Magufuli,” alisema Profesa Lumumba.

Alisema lazima mafisadi watachukia jinsi anavyoendesha Serikali yake, lakini akamtaka asife moyo kwani kwa anayoyafanya hawezi kupendwa na watu wote.

“Kumbukeni mafisadi ni watu wa ajabu, mtu mmoja ana nyumba 40, magari 20 na mwingine unakuta anamaliza mwaka hajatembelea baadhi ya magari yake, huo ni ujinga tu, ni ulafi, ni unguruwe huo.

“Tunataka viongozi watakaoboresha miundombinu, kilimo, maisha ya wanawake na watoto. Mwafrika anataka chakula kizuri, shule, hospitali nzuri na ajira kwa vijana,” alisema.

Kuhusu sakata la mchanga wa madini, Profesa Lumumba alisema Rais Magufuli yuko sahihi kwa anachokifanya.

“Nilisoma magazeti ya Tanzania, kwamba bosi wa Acacia alikwenda Ikulu akasema nimekosa sana na Rais Magafuli akamwambia nimekusikia mwanangu, tutakuhurumia, lakini kwa masharti na lazima ulipe fedha ulizopora,” alisema Profesa Lumumba.

Pamoja na hayo, aliwatahadharisha viongozi kuacha kujiona miungu watu kwani hali hiyo inachangia mdororo wa kisiasa na kiuchumi.

Hayo yote yamejiri wakati wa Kongamano la 9 la Kigoda cha Mwalimu Nyerere linaloendelea katika Chuo kikuu cha Dar es salaam, UDSM.

 

Posted By

-

Leave a comment

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>