Published On: Thu, Jun 8th, 2017
World | Post by jerome

MAHAKAMA YA RUFAA KENYA KUTOA UAMUZI WA UCHAGUZI WA UBUNGE

Share This
Tags

Mahakama ya rufaa nchini Kenya Juni 23 itatoa uamuzi kuhusu ikiwa matokeo ya urais yatakayotangazwa katika maeneo ya bunge ndiyo yatakayokuwaya mwisho au yanaweza kutathminiwa upya na Tume ya Uchaguzi.

Tume ya Uchaguzi ilikata rufaa baada ya Mahakama Kuu kuamua kuwa matokeo yanayotangazwa katika maeneo ya bunge yawe ya mwisho, lakini Tume inadai kuwa hali hiyo inaweza kuzua hitilafu.

Muungano wa upinzani NASA, unataka uamuzi wa Mahakama kuu usibadilishwe na umetishia kutoshiriki katika uchaguzi wa Agosti ikiwa uamuzi huo utabadilishwa kwa madai kuwa, unaweza kuzua udanganyifu wakati wa kujumuisha matokeo ya mwisho.

Viongozi wa upinzani Musalia Mudavadi, Kalonzo Musyoka, Raila Odinga, Moses Wetangula na Nick Salat waliungana, Januari 11, mwaka huu Jijini Nairobi.

Hata hivyo, Tume ye Uchaguzi inasema, kwa sababu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ndiye aliye na uamuzi wa mwisho wa kutangaza matokeo ya urais, ana jukumu la kuyapitia kuhakikisha kuwa yamekamilika kabla ya kuyatangaza.

Wakili wa upinzani James Orengo, amesema kuna uwezekano mkubwa wa matokeo ya mwisho kubadilishwa na Tume ya Uchaguzi ikiwa, matokeo kutoka maeneo bunge hayataheshimiwa.

Mwanasheria Mkuu wa serikali Githu Muigai na Mawakili wa Tume ya Uchaguzi wamewaambia Majaji wa Mahakama hiyo kuwa, Mwenyekiti wa Tume ambaye kwa sasa ni Wafula Chebukati, amepewa mamlaka ya kutangaza matokeo ya mwisho ya urais.

Majaji Asike Makhandia, Kathurima M’inoti, Patrick Kiage, William Ouko na Agnes Murgor, ndio wanaosikiliza kesi hiyo wakati huu kampeni za kisiasa zikiendelea kushika kasi.

Posted By

-

Leave a comment

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>