Published On: Tue, Apr 4th, 2017
Sports | Post by jerome

ROGER FEDERER KIDUME UBINGWA WA MIAMI OPEN

Share This
Tags

Inaweza kuwa ajabu lakini ni kweli. Mcheza tennis Roger Federer katika umri wa miaka 35 amefanikiwa kutwaa ubingwa wa Miami Open kwa kumfunga mpinzani wake mkubwa Rafael Nadal kwa seti 6-3, 6-4.

Akiwa kama nyoka, anavyozeeka ndivyo sumu inavyozidi kuwa kali, Federer amemfunga Nadal mara tatu mfululizo kwa mwaka huu huku pia ikiwa na maana kuwa ameweza kushinda mataji matatu kwa mwaka huu.

Ukwasi huu wa mataji kwa Federer kwa mwaka huu ulianza kwa yeye kufanikiwa kuchukua taji la Australian Open mwezi January ambapo alimfunga Nadal katika fainali, akatwaa pia taji la Indian Wells wiki kadhaa zilizopita kabla ya kutwaa taji la Miami Open.

Federer ameweka rekodi ya kuwa mtu mzima zaidi kuwahi kushinda Miami Open kwa kuwa na miaka 35, hii ikiwa ni rekodi kwenye miaka 33 ya historia ya shindano hilo.

Hata hivyo Federer ameweka wazi kuwa atapumzika kwa miezi miwili kwa sababu mwili wake sio wa kijana mwenye umri wa miaka 24 tena na anahitaji muda kupumzika.

Kwa kiwango chake na ikitokea akafika katika nafasi ya kwanza ya viwango vya ubora mwaka huu basi atakuwa amevunja rekodi ya mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi kushika nafasi hiyo.

Kwa upande wa wanawake, Johanna Konta alitwaa taji lake kubwa zaidi kwenye maisha ya Tennis baada ya kufanikiwa kumfunga mchezaji bora namba moja wa zamani Caroline Wozniacki kwa seti 6-4 6-3.

Konta ambaye alikuwa namba 145 kwenye orodha ya ubora mwaka 2015 mwezi June atapanda mpaka nafasi ya 7 kutoka nafasi ya 11 aliyokuwepo wakati anaingia kwenye mashindano haya ya Miami Open.

Posted By

-

Leave a comment

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>