Published On: Wed, Jan 6th, 2016

ZIDANE TIZAMA NYUMA YA MIWANI YA PEREZ NA MIGONGO YA MASHABIKI BERNABEU.

Share This
Tags

Mhasisi wa Taifa hili, hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere alifariki dunia 1999 Oktoba 14.

Huu ulikuwa takribani mwaka mmoja tangu Zinedine Zidane atwae taji la ubingwa wa dunia huku akifunga mara mbili katika fainali dhidi ya Brazil na ukiwa ni takribani mwaka mmoja pia kabla Zidane hajatwaa uchezaji bora wa mashindano ya mataifa ya Ulaya wakati Ufaransa ikitwaa ubingwa huo mwaka 2000 kwa kuichapa Italy.

Mchezaji ambaye pamoja na ukimya wake ndani ya uwanja miguu yake ilikuwa na kelele za aina yake na uongozi kwa wenzake ulianzia katika nyayo zake kuliko kichwa chake.Wakati waswahili wakiamini akili ni nywele, Zizou alikuwa akinyonyoka za mbele huku uwezo wake ukitamalaki katika mboni za macho ya walio wengi.

Nani asingependa kuona goli bora alilofunga dhidi ya Bayer04 Leverkusen? Ni kama ambavyo hata ikiwa ni miaka takribani 9 tangu astaafu vijana wengi wapenda soka wanakua wakijaribu kujifunza staili yake maarufu ya Marseille Turn au jina lingine Zidane Roulette.

Ni nadra sana kuziona nyakati zake katika miguu ya mchezaji mwingine hasa kipindi hiki ambacho mchezaji mbunifu zaidi wa Juventus ni Paul Pogba.Lakini wakati ukimya wake mbele ya kamera ukiondoka kwa Muda mrefu, moja ya binadamu wababe zaidi katika sayari ya tatu kati ya tisa zilizopo Florentino Perez amemrejesha mbele yetu.

Kamrejesha mbele yetu lakini kipindi hiki akiwa amemvisha suti ghali za Desmond Merrion, na kumfanya kuwa kocha mkuu wa klabu yenye historia kubwa ya Real Madrid. Inawezekana kabisa kuwa hii ingeweza kuwa kazi ngumu zaidi kwa mtu kuikubali katika kipindi hiki hasa mwajiri wako ukitambua kuwa ni Perez.

Mtu ambaye urafiki wake na watu hugota kwenye kuta za miwani yake. Mtu ambaye anajua kila asichokijua. Mtu ambaye anaamini soka ni mchezo rahisi sana na ni rahisi katika urahisi wake kiasi cha kuwaondoa Makelele na Alonso na kazi zao kufanywa na aina ya kina Toni Kroos.

Kwa Perez, Edo Kumwembe angeweza kufanya kazi ya Masoud Kipanya. Hajawahi kuwaza nani anafanya nini, na yupi anakaa wapi, lakini anachowaza ni nani atakuja vipi na mashabiki mtafarijika vipi.

Huu ni ukaidi ambao hawezi kuuacha na ambao mashabiki wa Madrid wanaupenda. Huyu ndiye pekee anayewafanya mashabiki waendelee kuamini kuwa hakuna timu kubwa kama Madrid hata isipotwaa mataji. Huyu ndiye pekee anayeweza kumtelekeza Casillas na hakuna atakayehoji.

Mtu pekee anayeweza kuilaza dunia nzima ikimtusi kwa maamuzi yake ya sekunde tano.
Ni kama ambavyo ardhi na mbingu zinavyomsonya kwa kumpiga kisu Rafael Benitez, kocha aliyetumia mdomo wake kusema ukocha wa Madrid ilikuwa kazi ya ndoto yake.

Tukio alilofanya Perez kwa Benitez lilikuwa linatabirika sana. Wengi wanaweza kujiuliza inakuwaje unamfukuza kocha ambaye yupo nyuma ya kiongozi wa ligi kwa pointi 4 pekee. Inakuwaje unamfukuza kocha aliyepoteza michezo 3 pekee kwenye ligi? Maswali ambayo yanajibiwa na maneno mawili tu Zinedine Zidane.

Akilini mwa Perez alikuwepo Zidane kabla ya Pellegrin kuifundisha Madrid mwaka 2009. Kipindi hiki aliamua kumpa cheo cha uongo Zidane kuwa mshauri wake mkuu wa masuala ya soka. Kipindi hiki alikitumia kumwandaa Zidane kuja kuwa kocha wa baadae wa Madrid. Akampa ukocha wa timu ya vijana ya Castilla, akampendekeza kuwa msaidizi wa Carlo Ancelloti.

Wakati anafukuzwa Ancelloti, Perez alitumia akili nyingi kuliko ile ambayo John F Kennedy alitumia kuwabana Cuba na Urusi. Alijua fika ungekuwa mzigo mkubwa sana kumpa timu Zidane baada ya Carlo Ancelloti. Alitaka mtu atakayekaa katikati yao. Hakuna ambaye hakujua kuwa Benitez alikuwa kapewa mzigo mzito.

Hakuna ambaye hakuwaza kuwa Benitez hakuwahi kufundisha timu ambayo haina kiungo mkabaji wa asili.
Benitez aliajiriwa ili afukuzwe ingawa hii imekuja mapema sana. Benitez alikuja kama utangulizi wa filamu iliyokuwa inaandaliwa kichwani mwa Perez.

Perez hakupanga kuiachia mapema hivi lakini imembidi. Kwake tatizo sio nafasi iliyopo Madrid, lakini ni kwa namna gani Denis Cheryshev anaweza kupata nafasi wakati Isco yupo benchi. Tatizo kubwa kwake ni vipi mchezaji wake James Rodriguez anakaa benchi wakati Kovacic anapata kadi nyekundu na timu inasuluhu dhidi ya Valencia.

Bahati mbaya kubwa ni kuwa Benitez alishindwa kuendesha chumba cha kubadilishia nguo cha Madrid. Inasemekana hata kwenye viwanja vya mazoezi alikuwa anakutana na kejeli cha Kina Ronaldo, Marcelo, Ramos na James.

Ancelloti alifanikiwa kukishika chumba kwa kuwafanya wachezaji kuwa marafiki, Mourinho alifanikiwa kukifanya chumba kiamini kuwa ni vita kati ya Madrid dhidi ya dunia iliyosalia. Lakini Benitez hana tabia hii, hafanani na yeyote kati ya hawa. Hakuwahi kuwa kocha anayewajali wachezaji nje ya uwanja.

Huwezi kubaki salama kwa namna hii mbele ya Perez. Wakati huu ambao Barcelona inaongozwa na MSN ni kipindi kigumu sana kwa mtu yoyote anayeichukua Madrid. Umefika wakati wa Zidane Sasa, wakati muafaka wa kujua akili ya Perez. Zidane analeta kitu kipya ndani ya Madrid.

Anakuja kama kocha ambaye wachezaji wote wanahusudu alichokifanya akiwa mchezaji, Benitez hakuwahi kuwa mchezaji wa kiwango cha juu. Pamoja na ukimya wake, Zidane anaweza kurejesha furaha ya wachezaji wa Madrid. Ni rahisi sana kwa Zidane kumkanya au kuzungumza na Ronaldo kuliko Benitez.

Ni rahisi sana kwa Zidane kumwambia Isco hujui unalofanya na Isco akawa anaamka asubuhi na mapema kupandisha kiwango chake. Analeta sura mpya ndani ya vyumba vya kubadili nguo. Nafurahi kuona kuwa anafanya kitu ambacho wachezaji wachache waliocheza soka kwa kiwango cha juu wamethubutu kufanya.

Ni safari mpya, safari ya kupitia jangwani huku ukiwa na akiba ndogo ya maji. Tofauti na zamani, Sasa hivi atapoteza Muda mwingi akiwa na Ramos kuliko Perez. Perez atakaa jukwaani akisafisha miwani yake.

Urafiki wao pia utakuwa unagota kwenye kuta za miwani hiyo, huku akichungulia kuona kama mashabiki wa Bernabeu wanashangilia kwa nguvu.

Msimu uliosalia unaweza kuwa kipimo kwa Zidane lakini unaofuata kama akisalia utakuwa shubiri. Zidane ameishi akipendwa na mashabiki kwa kipindi chote, lakini wakati huu usaliti upo jirani zaidi. Upo nyuma ya miwani ya Perez, upo migongoni mwa mashabiki wa Madrid. Tunataka tu kuamini hautakuwepo, lakini kwa Perez usaliti ni tabia njema mbele ya Madrid.

Posted By

-

Leave a comment

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>