Published On: Fri, Jan 8th, 2016

UHARIBIFU WA MAZINGIRA NA TISHIO LA KUTOWEKA ZIWA MANYARA

Share This
Tags

ZIWA Manyara ni miongoni mwa maziwa ambayo yamekuwa kivutio kikubwa kwa wageni wa ndani na watalii kutoka nje ya nchi wanaotembelea katika Hifadhi ya Taifa ya Manyara kutokana na uzuri iliyokuwa nayo.

Miongoni mwa vivutio vikubwa ndani ya ziwa hilo ni pamoja na wanyama wa aina mbalimbali ikiwemo kiboko, ndege wazuri wa aina mbalimbali kama korongo pamoja na uwanda mkubwa uliojaa wanyama tofauti huku wakionekana kwa mbali wakila majani na wengine kusogelea ndani ya ziwa kwa ajili ya kunywa maji. Maji ya moto yanayotokea chini ya ardhi yenye uwezo wa kuchemsha yai na kuiva pia ni sehemu ya vivutio vinavyopatikana ndani ya hifadhi ya Manyara ambapo uongozi wa hifadhi umeweza kujenga eneo hilo na kuongeza ubora zaidi.

Simba wanaopanda juu ya miti ambao wanapatikana pekee katika hifadhi ya Manyara ni kivutio kingine kikubwa kwa watalii wanaotembelea eneo hilo. Hata hivyo mbali ya vivutio vyote hivi, kumekuwa na tishio kubwa la kutoweka kwa Ziwa Manyara na kubakia historia kufuatia kila kukicha eneo lake la ziwa kuendelea kuwa dogo pamoja na kina chake kujaa uchafu wa aina mbalimbali ikiwemo matope na mawe.

Wataalamu wamekuwa wakihaha huku na kule kuweza kubaini tatizo hilo limekuwa likisababishwa na nini ili kuweza kulipatia ufumbuzi na hatimaye kunusuru hali hiyo ambayo hakika ni tishio kwa maslahi ya wengi. Hata hivyo kikubwa ambacho kinaweza kuonekana kuwa ndio suluhu halisi ya tatizo la Manyara ni kuzuia uharibifu mkubwa wa mazingira unaofanywa na wakazi wa maeneo yanayozunguka ziwa hilo.

Baada ya utafiti wa muda mrefu pamoja na uzoefu wa kutosha kuhusiana na Ziwa Manyara, uongozi wa Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara unasema elimu ya matumizi bora ya ardhi kwa wakazi wa vijiji zaidi ya 40 vinavyozunguka eneo la hifadhi hiyo, ndio inaweza kuwa njia pekee ya kuzuia kutoweka kwa ziwa hilo. Kaimu Mhifadhi wa Hifadhi ya Ziwa Manyara, Marko Meoli, anasema ukubwa wa ziwa hilo lililoko katika uwanda wa bonde la ufa umeendelea kupungua kwa kasi kubwa kufuatia kujaa mawe, matope na takataka nyingine zinazotoka katika vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo.

Meoli anasema baada ya kugundua kuwa uharibifu wa mazingira unaweza kuwa tatizo la kutoweka kwa Ziwa Manyara kwa vipindi tofauti uongozi wa hifadhi hiyo umekuwa ukitoa elimu ya matumizi bora ya ardhi kwa vijiji hivyo vinavyozunguka Hifadhi ya Manyara. Hata hivyo Meoli anasema pamoja na kutoa elimu hiyo bado uharibifu wa mazingira umeendelea kufanywa na uchafu zaidi kuendelea kujaa ndani ya ziwa hali ambayo inatoa mwanya kwa wanasayansi watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi cha Mandela kilichopo Tengeru jijini Arusha kutaka kufanyia utafiti ukubwa wa tatizo katika ziwa hilo.

“Pamoja na jitihada zote ambazo tumekuwa tukifanya kuhakikisha tunazuia uharibifu zaidi ndani ya ziwa bado udongo umeendelea kujaa lakini hata hivyo tumeshindwa kujua ukubwa halisi wa tatizo licha ya kuona kwa macho kwa kuwa unahitajika utaalamu wa hali ya juu kujua hilo,” anasema Meoli. Anasema wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi cha Mandela kilichopo Tengeru, jijini Arusha, wako mbioni kufanya utafiti wa sababu ya tishio la kupungua kwa ukubwa wa Ziwa Manyara.

Pengine majibu yao yanaelezwa kuwa yataweza kuwa suluhu tosha ya tishio la kutoweka kwa Ziwa Manyara ambalo linaelezwa kuwa katika historia ya kipekee Afrika na duniani. Hata hivyo Muikolojia kutoka Mamlaka ya Hifadhi za Taifa, Yustina Kiwango, anasema katika utafiti walioufanya kupitia hifadhi ya Manyara waliweza kugundua kuwa ukosefu wa makinga maji kwa wakulima jirani na hifadhi hiyo ni sababu ya kujaa kwa Ziwa Manyara.

Anasema wakulima wanaozunguka hifadhi ya Manyara wamekuwa wakisababisha mmomonyoko wa udongo kwa kulima bila kuweka makinga maji ambapo mifereji inayopita pembezoni mwa matuta hayo hutiririsha maji kuingia ziwani ambayo pia hubeba udongo. Kiwango anasema kiwango cha udongo unaoingia ndani ya Ziwa Manyara ni vigumu kukijua kwa kile anachosema kuwa eneo hilo liko katika mkondo wa bonde la ufa hivyo limekuwa likititia kila mara kutokana na tetemeko la mara kwa mara linalotokea.

Anasema labda ujio wa watafiti katika Chuo Kikuu cha Mandela unaweza kuleta majibu ya ukubwa wa tatizo hilo na hatimaye kujua njia sahihi na hatua madhubuti za kuweza kukomesha tatizo hilo. Kiwango anasema yeye kama mwanasayansi, vipimo ambavyo anaweza kuvipata kutokana na wingi wa udongo na uchafu ndani ya Ziwa Manyara hatoruhusiwa kuchapisha popote kwa kuwa sio halisi kutokana na vifaa atakavyotumia kutohimili jiografia ya eneo la Ziwa Manyara ambalo hutitia kila mara na kupoteza uhalisi wa vipimo.

“Wakulima wanaolima pembezoni mwa Mlima Kilimanjaro wamekuwa wakitumia makinga maji kuendesha kilimo chao na ndio maana hujawahi kusikia kutokea kwa mmomonyoko wa udongo Kilimanjaro, ni tofauti kabisa na wakulima wanaozunguka hifadhi ya Manyara….hili la kujaa udongo labda watafiti wa Chuo Kikuu cha Mandela watafanikiwa,” anasema Kiwango. “Pia tabia mbaya ya kukata miti na kutopanda miti imekuwa ikisababisha mmomonyoko wa udongo katika eneo la Ziwa Manyara, endapo tabia hii haitakomesha tatizo halitaweza kuisha,” Kiwango anaeleza.

Anasema miti zaidi ya 15 iliyokuwa ikianzia katika vijiji vinavyozunguka Hifadhi ya Manyara kutiririsha maji ndani ya ziwa imekauka na kubakia mito mitano pekee katika kipindi cha miaka hamsini nyuma. “Kwa hiyo kwa haraka haraka tunaweza kusema matumizi ya maji kwa kilimo na mifugo, ongezeko la watu na mwisho kabisa ukame wa mara kwa mara vimechangia kwa kiasi kikubwa kukauka kwa Hifadhi ya Manyara,”anasema Kiwango.

Kiwango anasema vitendo vyote hivyo hapo juu ukiachia suala la ukame vitaweza kudhibitiwa endapo halmashauri za vijiji husika zitatunga sheria ndogo ndogo (by laws), za kudhibiti uharibifu wa mazingira kwa kufuata sheria ya ardhi inayotaka kuchukuliwa tahadhari kwa wakulima wanaolima maeneo ya miinuko. Mbali na kutoa elimu hiyo, akizungumza wakati wa kilele cha maadhimisho ya sikukuu ya Uhuru, Kaimu Mhifadhi wa hifadhi hiyo, Marko Meoli anasema usafi ni sehemu ya kazi za kila siku katika Hifadhi ya Manyara.

Anasema usafi ni sehemu ya utalii kwa kuwa bila kufanya usafi katika maeneo yanayozunguka hifadhini wageni watapata maradhi ya kuambukiza na hawatatembelea maeneo hayo tena. “Bila usafi hakuna mgeni atakayenunua bidhaa yoyote na hatoweza kutembelea hifadhi yetu, wakazi wa hapa Mto wa Mbu wanauza vinyango na urembo kwa watalii, ni lazima kufanya usafi ili waweze kufanya biashara zao,” anasema Kiwango.

Anasema Hifadhi ya Ziwa Manyara imekuwa ikishirikiana na wakazi wa vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo kuhakikisha maeneo ya hifadhi yanakuwa safi wakati wote ili kuepuka magonjwa kwa wanyama na binadamu. Meoli anatoa wito kwa Watanzania kutembelea Hifadhi ya Ziwa Manyara kwa bei rahisi wakati huu wa sikukuu na kujionea vivutio mbalimbali vilivyopo ndani ya hifadhi hiyo na kwamba hawatajutia matembezi yao katika hifadhi hiyo.

Seif Mangwangi ni mchangiaji wa makala katika gazeti hili

CHANZO: HABARI LEO

Posted By

Leave a comment

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>