Published On: Wed, Jan 6th, 2016

SAMATTA CHUKUA POCHI YA KATUMBI USIITAMANI KALAMU YAKE.

Share This
Tags

Katumbi ni mtu wa pili kwa umaarufu na nguvu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Anazidiwa kwa kiasi kidogo sana na Rais wa nchi hiyo Joseph Kabila. Lakini upande anaoupenda yeye sio siasa sana, ni muumini mkubwa wa biashara.

Kila anachokiona kwake anakitizama kwa upande wa faida yake. Kikimlipa anakipenda kwa moyo wake wote, anakithamini kisha anakitunza, baadae mapenzi yanazidi na anashindwa kukiachia.

Bahati mbaya sasa kahamia katika rasilimali watu. Anamiliki timu Kisha anamiliki wachezaji wake. Anawalea wanavyotaka, anawapa ufalme kisha anawafanya matajiri.

Ukishakuwa nyota anakufanya jirani yake, anakulipa kwa kila goli unalofunga kisha anakufanya uamini kuwa Kuna maisha mazuri sana nje ya Florentino Perez. Anakupa uhakika wa kuishi kifahari kuliko wachezaji wengi wanaocheza ligi kuu ya Ufaransa.

Bahati nzuri yeye hana maisha ya Johannesburg, hana maisha ya soka la ndani. Anapenda kuwafanya Waarabu waamini Kuna ushindani nje ya kule kaskazini kisha anashinda ubingwa wa klabu bingwa Afrika. Anakupa uhakika wa kubadilishana jezi na Messi mwezi Desemba kwenye klabu bingwa dunia. Unapata kiburi cha Mputu, umaarufu wa Kidiaba kwa sababu ya pochi yake nene.

Pochi yake haijawahi kuwa tatizo kwangu. Sijawahi kukwazika na ununuzi wake wa ndege. Wakati anajenga uwanja wa thamani ya paundi milioni 35 nilitambua fika aliamua kuweka mabadiliko kwenye soka la Afrika.

Alifanya uwekezaji ambao ni rahisi kufanyika katika klabu kongwe za simba na Yanga kipindi ambacho shabiki wa Tanzania atajua tofauti ya soka la mapenzi na soka la uwekezaji. Tatizo kwa Katumbi na mimi ni kalamu yake tu. Kalamu yake ina akili sawa na medulla yake.

Kalamu yake haijawahi kwenda kinyume na yeye. Kila wino unaodondoka kutoka kwenye mdomo wa kalamu hiyo unazungumza vitu vipi tu, Tp Mazembe na Moise Katumbi. Ni kalamu hii ndiyo ilimrejesha Patou Kabangu kutoka Anderlecht mpaka Tp Mazembe.

Ni kalamu hii iliyotaka kukwamisha usajili wa Alain Dioko Kaluyituka kuelekea katika klabu ya AL Ahly Doha ya Qatar. Ni kama ambavyo kalamu hii inanipa hisia kuwa inataka kumlambisha ardhi mchezaji Mbwana Samata maarufu kama Samagoal kwa wakongo.

Kalamu hii ishanusa upande wa pili wa karatasi za Samata. Inataka kuangusha wino ambao imezoea kuangusha. Wino wa kumfunga mchezaji au wa kumpa faida anayeimiliki Moise Katumbi. Wakati Watanzania wakiwa na furaha, Katumbi amenuna. Amenuna hasa.

Samata alishaamua hatobaki Mazembe. Samata alishaamua kuikwepa pochi nene ya Katumbi. Maisha yake ya soka alishajua yanavuka mipaka ya Afrika. Kipaji chake maridhawa alihitaji kiwe jirani na Aubameyang.

Wakati Samata anapanga yote haya, Katumbi alikuwa kalala amekumbatia kalamu yake maridadi. Akaifuata kalenda akagundua Samata alikuwa hana zaidi ya miezi sita kwenye mkataba wake. Akasubiri kujua nini kitatokea. Akaivaa akili yake iliyomfanya kuwa milionea akavua upenzi wa soka.

Kwake yeye kwa Sasa alihitaji mikono ya Samata kuliko miguu yake tena. Genk walivyogonga hodi Samata akawakaribisha kama tu ilivyo katika maandishi kuwa bisheni hodi nanyi mtafunguliwa.

Kipindi hiki alijua Fifa na Caf wanamruhusu kabisa kuzungumza na klabu yoyote anayoitaka hata ikiwa ni kimondo ya Mwashiuya.

Akasaini mkataba wa awali na akawang’ata sikio Genk kuwa harudi Mazembe . Genk kama ilivyokuwa vilabu vinavyojielewa vya kimataifa vikaomba kukutana na Mazembe. Katumbi akawepo ambaye ndiye Mazembe yenyewe, wakamwomba kumchukua mwezi Januari.

Katumbi kama mshambuliaji bora wa kibiashara akavaa kalamu yake, akawaonyesha Genk medali za Samata, akawaonyesha nyimbo anazoimbiwa, pesa anayolipwa Kisha akawaletea video za mitaani pindi Samata anapopita. Akamalizia kwa kuwaambia mfalme anaondoka kwa Euro million 2.5.

Waliposita akashuka mpaka million 1 waliposita tena akang’ata kalamu yake, akawaambia wazungumze. Wao kwa kutambua watampata bure dirisha la kiangazi wakasema wanatoa euro laki 7. Katumbi akavaa kofia yake, akaificha kalamu yake Kisha akawaacha na kahawa zao mezani.

Inasemekana mawazo ya utulivu hupatikana bafuni. Akakumbuka kuwa tofauti na kalamu Kuna pochi nene kwenye mifuko ya nyuma ya suruali. Akatuma mwakilishi kwa Samata, kisha akawawahi Genk kabla kahawa haijaisha. Akaja na mbinu za Simba na Singano, akasema Samata aliongeza mkataba wa mwaka mmoja mpaka 2017.

Genk wakacheza mchezo wa chess yeye akacheza draft, michezo ya kuviziana huku unawaza sana. Alipogeuka nyuma akapata ujumbe mfupi wa salamu kutoka kwa rafiki yake wa klabu ya Standard Liege.

Akaondoka zake na hotel aliyokuwamo akarejea kwake. Akamtambulisha kijana kwa Standard Liege, wakamtamani na wakakubaliana na dili la kalamu yake.

Tatizo ni Samata kuvunja mkataba wa awali na Genk. Tatizo lingine likawa ni wapi Samata anapataka. Katumbi yupo tayari kugombana na Samata ili kalamu ifanye kazi yake. Hii ni tabia ya matajiri wengi sana, kalamu huwa na umuhimu kuliko pochi. Wino wenye sahihi huwa mwamuzi wa mwisho.

Bahati nzuri ya Samata ni kuwa mkataba wake unamweka Katumbi katika ugumu. Ingawa Samata kashika mpini lakini Katumbi hajajali kushika makali, kwake kwa Sasa anahitaji sahihi ya Samata kuliko magoli yake ya baadae. Anataka kupata pesa ya kuleta akina Rodger Asale wengine huku akiongeza uwanja wa mazoezi.

Wakati Samata pengine akiingia kwenye harakati za Che Guevara bado napata shaka na akina Ulimwengu na wanaomfuata Katumbi, Ubwa na Chanongo. Napata shaka kama wanajua kutofautisha kati ya pochi yake na kalamu yake. Kalamu iliyowalaza pale Mazembe Kalaba na Singuruma.

Wakati nikikumbuka akili za wachezaji wetu katika sakata la kalamu za matajiri mwili unanisisimka. Nikimkumbuka Mwashiuya au Singano, machozi yananitoka. Natamani tupate darasa la namna ya kushika kalamu. Acha nianze na Ulimwengu, Kaka ni sahihi wewe kuitumia pochi ya Katumbi lakini usiitamani kalamu yake. Ukikosea tu, Ufaransa itakuwa umbali wa sayari ya Pluto.

Posted By

-

Leave a comment

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>